Dar/mikoani.
Baadhi ya vituo vya mafuta vimefunguliwa na vingine kuendelea kufungwa katika
maeneo ya jiji la Dar es Salaam na mikoa mbalimbali kutokana na sakata la
mashine za kieletroniki za stakabadhi zilizounganishwa na pampu (electronic
fuel fiscal printer).
Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), juzi ilivifungia vituo vya mafuta kote nchini
vilivyoshindwa kufunga mashine hizo za kutolea stakabadhi.
Jana,
baadhi ya vituo vilionyesha ushirikiano kwa TRA kwa kufanya utaratibu wa
kununua mashine hizo na vikaanza kufanya kazi kama kawaida.
Kati ya
vituo vya mafuta 71 vilivyofungwa jijini Dar es Salaam, 52 vilitoa ushirikiano
kwa mamlaka hiyo na vilitarajiwa kufunguliwa muda wowote ili kuendelea na
huduma.
Waandishi
wa gazeti hili walizunguka katika vituo mbalimbali vya kuuzia mafuta jijini Dar
es Salaam na kukuta misururu ya magari ikiwa imepungua ikilinganishwa na hali
ilivyokuwa juzi.
Hata
hivyo, katika baadhi ya mikoa hali ilionekana kuendelea kuwa ngumu.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo alisema kazi ya kuvifungia
vituo hivyo itaendelea nchi nzima hadi pale agizo la utumiaji wa mashine hizo
litakapotekelezwa.
Kwa Wilaya
ya Kinondoni vituo 28 vimefungwa, Ilala vituo 31 na Temeke vituo 12.
Hata
hivyo, Kayombo alisema TRA imeanza kuvifungulia vituo vilivyofungwa pindi
vinapotimiza masharti na kufuata taratibu za kuwa na mashine hizo kama
inavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema si
lengo la TRA kuwaumiza wananchi au kuwasumbua wafanyabiashara bali ni
utekelezaji wa sheria na taratibu zilizowekwa na kupitishwa na Bunge.
“Tunaomba
wananchi wawe wavumilivu katika kipindi hiki ambacho tunataka sheria na
taratibu zifuatwe kwa wafanyabiashara kutumia risiti hizo kama ilivyoanishwa
kisheria na kutangazwa bungeni,”
“Wanaotimiza
masharti watafunguliwa haraka iwezekanavyo ili waendelee kutoa huduma na
kuwaondolea wananchi usumbufu usiokuwa na msingi,” alisema.
Pia,
Kayombo aliwataka wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwa kutafuta mashine hizo
kwa kuwa ndiyo utaratibu unaotakiwa kufuatwa.
Kuhusu
gharama za mashine hizo kuwa juu, Kayombo alisema si kweli na wafanyabiashara
walipewa muda mrefu kwa ajili ya kujiandaa, lakini hadi sasa bado wapo ambao
wanataka kuendelea kufanya biashara bila kutoa risiti halali.
“Kuna
wasambazaji watano wa mashine hizo, unaweza kumchagua yeyote ambaye utaona
gharama zake zina nafuu kwetu jambo la muhimu uwe na mashine hiyo,” alisema.
Julai 13,
TRA ilianza kufungia vituo ambavyo havijaweka mashine za stakabadhi
zilizounganishwa na pampu (electronic fuel fiscal printer).
Hatua hiyo
ilianza siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuzuru
katika kituo kimoja cha mafuta kilichopo eneo la uwanja wa ndege na kukuta
huduma zinatolewa bila risiti, hivyo akaamuru kifungwe.
Dk Mpango
alisema kufanya biashara bila risiti za EFD ni wazi wafanyabiashara wana lengo
la kuiibia Serikali.
Wanunua
mafuta Kenya
Wilayani
Tarime, TRA imeendelea kufunga vituo vya mafuta, hali ambayo imesababisha
usumbufu kwa watumiaji ambao wamelazimika kutembea umbali wa kilomita 18 kwenda
wilaya jirani ya Sirari au kuvuka mpaka kwenda nchini Kenya kupata huduma hiyo.
Wakizungumza
na gazeti hili, watumiaji hao wamesema pamoja na kusafiri umbali huo, huduma
hiyo imeadimika katika maeneo hayo hali inayosababisha wanaouza rejareja
kupandisha bei kutoka Sh2,500 hadi Sh3,000 kwa lita.
Hali
kadhalika usafiri wa bodaboda nao umepanda bei kutoka Sh1,000 kwa bei ya
kawaida na kufikia Sh2,000 au zaidi ya hapo ikitegemea na umbali.
Mkazi wa
Mtaa wa Rebu Senta wilayani Tarime alisema gharama hizo zilipanda saa chache
baada ya TRA kufungia vituo vingi vya mafuta.
Mabadiliko
ya bei hizo yamekuja baada ya vituo saba kufungiwa kutokana na kutokidhi
vigezo.
Halikadhalika
wilayani Musoma wananchi wameendelea kupata adha ya usafiri baada ya nauli
kupanda kutoka Sh2,000 hadi Sh5, 000 kutoka mjini hadi Bweri kwa pikipiki.
Meneja wa
TRA wa mkoa, Ernest Nkang’aza ameonya watakaokwenda nchi jirani kujaza mafuta
kuwa watachukuliwa hatua kwa kuwa watu wa uhamiaji wanawafuatilia.
“Vituo
vyote vitaendelea kufungwa hadi pale wamiliki watakapofunga mashine hizo,”
alisema Nkang’aza.
Tatizo
hilo la mafuta pia limeugusa mkoa wa Tabora ambako vituo 21 vimefungwa katika
wilaya za Tabora Mjini vituo vinne, Igunga vinne Urambo na Nzega vituo vitano
huku fungiafungia hiyo ikihamia wilaya za Sikonge na Kaliua.
Akizungumzia
suala hilo, meneja wa mkoa, Leonard Shija alisema kazi hiyo si ya kushtukiza
kwa kuwa wamiliki walipewa muda wa kutosha, hivyo watahakikisha vituo vyote
visivyotekeleza agizo hilo, vinafungiwa.
Katika
Mkoa wa Kagera, vituo sita wilayani Bukoba vimefungwa huku meneja wa mkoa, Adam
Ntoga akisema wamiliki wameshindwa kutimiza wajibu wao kwani walipewa muda
tangu Septemba mwaka jana.
Baadhi ya
watumiaji wa vyombo vya moto , hasa bodaboda, walisema kufungiwa kwa vituo
hivyo kumewaathiri kwa kuwa wamelazimika kufuata mafuta Kyaka na Kihanga kwa
watu binafsi huku bei yake ikipanda kutoka Sh2,400 hadi Sh 4,000 kwa lita.
Nyongeza na Elizabeth Edward
Saa 48 zilivyoacha machungu ya petroli na dizeli kila kona
Reviewed by Erasto Paul
on
July 16, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili