Vinara wa ufaulu kidato cha sita waeleza siri ya mafanikio

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Feza boys wakimbeba mwezao,  Fransic Samkyi kwa kuwa mwanafunzi bora kitaifa kwa masomo ya Sana kwa matokeo ya kidato cha sita 2016 yaliyotangazwa jana .Picha na Said Khamis 

Kwa kuwa anashinda akiperuzi katika mitandao ya kijamii kila siku, anaangalia tamthilia azipendazo bila kukosa, usidhani hasomi kwa bidii.

La hasha! Francis Samkyi, licha ya tabia hizo, lakini ndiye aliyeongoza kitaifa kwa upande wa wavulana akifanya vizuri katika masomo ya Sanaa katika matokeo ya kidato cha sita
Mwananchi lilikwenda nyumbani kwao, dakika chache tu baada ya matokeo kutoka yakionyesha kuwa shule yake ni miongoni mwa kumi bora na pia yeye ameongoza katika masomo ya Sanaa, kwa upande wa wavulana.
“Nimefurahi sana kusikia matokeo haya ila jambo la msingi kwangu nimekuwa nikizingatia nidhamu ya ratiba zangu za masomo, nipo katika mitandao ya kijamii kila mara lakini siyo kwa muda mwingi, ninapopumzika pia huangalia sinema na miziki,” alisema Fransis mwenye uso wa upole na tabasamu kwa mbali.
Ni mtoto wa tatu kati ya watoto wanne wa Mzee Thomas na Victoria Samkyi.
Thomas alisema licha ya kufanya kazi za nyumbani, wamemwachia muda kila siku ili kutekeleza ratiba yake ya kujisomea.
“Elimu ni uwekezaji, ukiwekeza matunda yake huonekana hapo baadaye, lakini ndiyo urithi wetu tunaoutoa kwa watoto. Tunaamini katika elimu zaidi,” alisema Victoria Samkyi.
Francis alimaliza darasa la saba katika shule ya msingi Academic International iliyopo Mikocheni mwaka 2000 na kushika nafasi ya kwanza kishule katika matokeo ya darasa la saba.
Kabla ya kujiunga Feza Boys, Francis alipata elimu yake ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Centennial Christian Seminary iliyopo Dar es Salaam mwaka 2014.
Wasichana waeleza siri ya mafanikio
Wanafunzi wawili wa kike wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Feza, (Feza Girls) Kabhabhela Bakuru na Atuganile Jimmy wametoa ya moyoni wakieleza kuwa kilichowawezesha kufaulu ni kujiepusha na mahusiano ya mapenzi shuleni.
Atuganile yeye ameshika nafasi ya nane kitaifa katika masomo ya Sayansi huku akishika nafasi ya tatu kwa wasichana katika masomo hayo ya Sayansi. Atuganile (20) ameyapokea matokeo hayo akiwa anaumwa homa ya matumbo (typhoid).
“Hapa nilipo ninaumwa na wakati napokea matokeo haya sikuwa kwenye hali nzuri. Ninamshukuru sana Mungu kupata daraja la kwanza, pointi 1.3 ya PCM, nilikuwa na wasi wasi na hesabu ilikuwa ngumu sana,” alisema Atuganile.
Atuganile ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne wa mzee Bakuru. Mama yake Happiness Mbuja ni Mhasibu wa Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi na baba yake Cairo Mbuja ni Mhasibu pia katika Kampuni ya Mufindi Mills Paper.
“Muda wa kujisomea ilikuwa ni ratiba, kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa nne nasoma na baadaye tena usiku kuanzia saa mbili hadi saa nne ninajisomea, ilikuwa ni lazima japokuwa pia nilikuwa mpenzi wa kuangalia sinema za mfululizo, taarifa ya habari na pia ninapenda muziki,” alisema.
“Kilichochangia ufaulu ni nidhamu katika matumizi ya muda wa ziada, kwenye ratiba za kujisomea, O level nilipata ufaulu mzuri tu kwa nafasi ya nane pia kama ilivyokuwa matokeo haya kitaifa,” alisema.
Kwa upande wa Kabhabhela ambaye analelewa na mama yake baada ya baba kufariki dunia, yeye ameshika nafasi ya saba kitaifa katika masomo ya sayansi kwa upande wa wasichana.
Kabhabhela alisema ufaulu wake unachangiwa na mambo mengi lakini muhimu ni nidhamu na kuzingatia masomo.
Mama yake ambaye ni mjane tangu mwaka 2012, ni mfanyabiashara wa kuuza vitenge katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Kabhabhela anayeishi Mbezi Juu, alisema hakuwahi kupitisha hata siku moja nyumbani bila kushika somo lolote kujisomea.
“Nyumbani tunaye msichana wa kazi ila pia kazi za ndani ninafanya, siko katika mitandao ya kijamii sana ila natumia WhatsApp pekee, kwa hiyo nilifanikiwa kuuzingatia muda wa kujisomea, familia yangu inamwamini Mungu nashukuru pia ilinilea katika mazingira ya kutokujichanganya sana na maisha mengine ya ujana,”alisema.
Kabhabhela amemaliza kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Marian Girls, pia amesoma elimu yake ya msingi katika shule hiyo hiyo.
Kwa nini Feza, Marian zinaongoza
Inawezekana umekuwa ukijiuliza ni kwa nini Shule za Sekondari za Feza ya Wasichana na ile ya Wavulana zimekuwa zikiongoza au kuwa katika shule kumi bora kila mwaka katika matokeo ya kidato cha sita.
Shule ya sekondari ya wasichana ‘Feza girls’ iliyopo Kawe imeongoza kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa jana.
Pia, imetoa mwanafunzi bora katika masomo ya Sanaa na wanafunzi walioingia katika kumi bora katika masomo ya Sayansi.
Fedha Boys iliongoza katika matokeo ya kidato hicho kwa mwaka 2015, ikashika nafasi ya pili 2016.
Akizungumzia siri ya shule hizo kufaulisha, Mkurugenzi wa Shule za Feza nchini, Ibrahim Yunus kupitia mahojiano yake na gazeti hili alisema ubora wa walimu walionao unatokana na hatua tatu kabla ya kumpata.
“Katika usaili, tunazingatia uwezo wa kufikiri, kujieleza, mwonekano wa mwalimu na maarifa yake,” alisema.
Yunus alisema kila mwaka shule hiyo inashiriki na kuandaa mashindano ya kitaifa na kimataifa katika masomo ya Sayansi, Hisabati, Tehama, midahalo ya kujieleza na biashara.
“Tunachozingatia zaidi ni ubora wa mafunzo tunayotoa kwa mwanafunzi na tunafuatilia ufaulu wake, wanafunzi wanaishi shuleni katika mabweni ila wachache tu wanaenda na kurudi,” alisema Yunus.
Alisema shule inapofungwa, wanafunzi hupewa majukumu ya kufanya wakiwa nyumbani na baada ya kurudi shule hukaguliwa ikiwa ni sehemu ya masomo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Marian Girls, Lightness Masawe alisema kufaulisha wanafunzi kunatokana na ushirikiano mzuri baina ya walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe.
“Tumeyafurahia matokeo haya kwa sababu ni darasa tulilokuwa tumeliamini, wanafunzi walionyesha bidii kwenye kusoma na walimu wakaonyesha jitihada katika kufundisha,” alisisitiza.
Alisema siri kubwa ya ufaulu wa shule hiyo ni bidii ya walimu katika kuwafundisha wanafunzi na kuhakikisha kila mmoja anasaidiwa kulingana na uwezo wake.
Mwalimu Masawe alisema kuwa mpango mzuri wa kazi waliojiwekea wa kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayeachwa nyuma kielimu ndio ambao umekuwa ukiwapa matokeo chanya kila wanafunzi hao wanapofanya mitihani yao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Marian Boys, Ihonde Joseph alisema siri kubwa ya mafanikio ya shule hiyo katika kufanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita ni nidhamu katika kila wanachokifanya.
“Kwenye shule yetu kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake na kufanya kazi kwa bidii. Walimu wanapotimiza wajibu wao, wanafunzi, wazazi na mameneja matokeo yake huwa ni kufaulu vizuri,” alisema.

Alisema wameyapokea matokeo hayo kwa furaha na kwamba, maandalizi mazuri waliyoyafanya waliamini kuwa wanafunzi wao wangefanya vizuri.
Vinara wa ufaulu kidato cha sita waeleza siri ya mafanikio Vinara wa ufaulu kidato cha sita waeleza siri ya mafanikio Reviewed by Erasto Paul on July 16, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.