Baraza la
Habari Tanzania (MCT), limepunguza vipengele vya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa
Habari (Ejat) kwa mwaka 2017 kutoka 19 hadi 14.
Kupungua
kwa vipengele hivyo kunatokana na sababu kadhaa ikiwemo rasilimali fedha za
kuendeshea tuzo hizo na zawadi.
Vipengele
vilivyopunguzwa ni tuzo za habari za kodi, ununuzi wa umma, Ukimwi na VVU,
habari za uchambuzi na matukio, na habari za afya ya uzazi wa mpango.
Katibu
Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ameeleza hayo leo Ijumaa wakati wa uzinduzi
wa tuzo za Ejat za mwaka 2017 mbele ya wanahabari.
Mukajanga
amesema mbali na changamoto ya rasilimali fedha, pia wameamua kupunguza
vipengele hivyo ili mashindano hayo yafanyike kwa ufanisi zaidi.
Amesema
vipengele vilivyobaki ni uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha;
habari za michezo na utamaduni; habari za afya na uandishi wa habari za
biashara na kilimo.
Tuzo
zingine ni za uandishi wa habari za elimu, utalii na uhifadhi, uchunguzi, data,
haki za binadamu na utawala bora, mpiga picha bora wa magazeti na runinga,
mchoraji katuni bora, habari za jinsia, wazee na watoto na kundi la wazi.
Mukajanga
amesema washindi katika makundi hayo watazawadiwa vyeti, tuzo na zawadi
nyingine.
Amesema
tuzo ya Mshindi wa Maisha katika Uandishi wa Habari itashindaniwa kwa mara ya
sita.
"Tuzo
hii hutolewa kwa mwandishi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha taaluma ya
uandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari," amesema.
Mukajanga
amesema tuzo za Ejat zitatolewa Aprili 27 mwakani na waandishi
wametakiwa kuwasilisha kazi zao kuanzia sasa hadi Februari 16 mwakani.
Amesema
kazi zinazotakiwa kushindanishwa ni zilizochapishwa na kutangazwa kati ya
Januari Mosi hadi Desemba 31 mwaka huu.
Waandaaji tuzo za Ejat wapunguza vipengele vya kushindaniwa.
Reviewed by Erasto Paul
on
October 06, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili