MJUE BLOGGER TUPOKIGWE ABNERY MWANDISHI WA KITABU CHA RIWAYA "MAPENZI KABURINI"



https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjIvi1GlhTN79QKUuwlP0WIxqH_68cooAD0HHaZ0KL97X4P7aGIqfxflehIoUL9ml42w2vj_k-CznF_fkfzLB5x_2rnVu0EwZTOf1hSEwkWCatIOQioBApTIQK6pYsSCl9_W8l8zUg56i4/s640/sinyati.jpg
Tupokigwe Abnery Mwampondele amezaliwa,Seronera - Serengeti mkoani Mara.Alisomea shahada ya Isimu ya lugha ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). 

Kwa sasa ni mwalimu wa somo la Kiswahili katika shule ya Sekondari ya Wasichana Precious blood iliyopo mkoani Arusha-Tanzania. N’je na kazi ya uwalimu Tupokigwe Abnery ni mtunzi wa vitabu vya hadithi, mbunifu wa mavazi ya kiasili, mjasiriamali na mwandishi wa gazeti tando (blogger) inayoitwa Sinyati Blog.

Tupokigwe Abnery alikuwa na kawaida ya kupenda kujibembeleza au kujifariji akiwa anatembea kwa kutengeneza hadithi katika fikra zake ili kuweza kulala au kufika anakoelekea bila kuchoka,ndipo siku moja baada ya kushiriki shindano la uandishi wa Riwaya fupi kwa wanafunzi wa shule ya msingi,sekondari na vyuo vikuu Tanzania kwa ajili ya Tuzo ya mama Salma Kikwete iliyoandaliwa na TASAKI(Tamasha la Sauti ya Kiswahili) aliibuka mshindi wa pili wa riwaya fupi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania.

Hivyo hiki kitabu ni muendelezo wa Riwaya aliyopatia Tuzo.Soma kitabu hiki uweze kujionea ubunifu wa hali ya juu wa fani pamoja na mshikamano wa maudhui uliyopo ndani ya kitabu hiki. 

Mapenzi Kaburini ni kitabu chenye mtazamo yakinifu,ni kitabu ambacho maudhui yake yamezitazama nchi za Afrika Mashariki na changamoto zilizopo katika nchi kwa upande wa viongozi pamoja na wananchi.Kimebeba maudhui yanayowalenga wananchi wote bila kujali utabaka.Kwa upande wa fani kimetumia majina ya halisi na kubuni hasa kwa upande wa maeneo ya miji mfano kuna miji kama Kinyonga,kupe,chatu ambayo ni majina yaliyopo katika nchi ya Simba.Nchi hii ya Simba ni nchi inayosimamia nchi zilizopo Afrika Mashariki.

Mbali na hilo pia visa na matukio vimepewa majina ya hifadhi za Taifa zilizopo katika nchi ya Tanzania.Mfano hifadhi ya Ruaha,Sanane,Manyara na kitulo kama ukisoma kitabu hiki utagundua kuwa sifa ya hifadhi inaendana na visa na matukio yaliyopo katika sehemu hiyo iliyoandikwa kwa jina la hifadhi.Mfano hifadhi ya Kitulo inasifika kwa kuwa na maua,kama tujuavyo maua huashiria sifa nyingi moja wapo hapo ni upendo,watu wengi hutumia maua katika kuwapa wapenzi wao,mfano kuomba msamaha,kumfariji mtu,hata kuonesha upendo kwa mtu unayempenda.

Utakaposoma kitabu hiki utaburudika na kufundishwa baadhi ya mambo kama Kukuza imani yako kwa Mungu,uaminifu katika ndoa,uzalendo katika nchi yako na Madhara ya kujihusisha katika mahusiano na mtu usiye mjua.
 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh4GTeskafJ11hg77OFtmCaat7XRn9kza2dxE81yML7PlQlJyas-usMUiJidB2ZSkjuEmoRE74RcqroIwXalysNFCR_2k757MFuDUZp3a9JK2unOwhznbSzngIJVgeI0tzZpHXSiR63Fec/s640/COVER+BOOK.jpg
  Nitakupatia kionjo kidogo katika sura ya kwanza ili kuweza kuona mwanzo tu wa hadithi hii ambayo hutapenda kuacha kuifuatilia:

Sura ya kwanza 

Hifadhi ya Sanane 
Ilikuwa siku ya Jumatatu katika ghorofa la tajiri mmoja, mmiliki wa hoteli maarufu katika nchi ya Simba. Tajiri huyo alifahamika sana kwa kuwa alikuwa akijitolea sana kwa wananchi wasiojiweza, katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.Watu husemamfadhili punda kuliko mwanadamu vilevile tenda wema kisha nenda zako baraka utazipata kwa Mungu,usisubiri hisani za wanadamu.

Pamoja na misaada aliyoitoa kwa watu mbalimbali lakini wananchi wa Simba hawakujali misaada yake, walimteta kila kona kuwa anatumia nguvu za giza na amekwisha toa kafara ndugu, jamaa na hata watoto wake ili kujipatia utajiri mkubwa alionao. Siku hiyo ya Jumatatu katika pagala la tajiri huyo aliyefamika kwa jina la Pesa nyingi.

katika moja ya chumba cha ghorofa hilo kulikuwa na mwanamke mrembo na mzuri sana wa sura, mrefu mithili ya twiga, mwenye umbo zuri la kiafrika, chini alikuwa amevaa suruali ya chupa huku akiwa amevaa blauzi tatu juu zenye rangi tofauti na nywele timutimu zikiwa zime nakishiwa na vitu vya jaani kama vichana,visude, rasta chakavu na kufungwa kitambaa cha kitenge aina ya makenzi ,uso wake ulikuwa kama paka mwenye madoa kutokana na kujipamba kwa majivu na masizi ya mkaa wa jaani. Pembeni ya ua hilo alikuwepo mnyama mwenye maringo 

mbugani kuliko wote, sio mwingine bali ni kijana mtanashati aliyekwenda hewaani, rangi ya ngozi yake nyeusi ya kung’aa. Tabasamu la mwanaume huyo lililokuwa likimfariji mtoto mzuri, lili mvutia sana Savannah. Ghafla ilisikika sauti ya mwanamke huyo ikiita kwa sauti ya chini iliyojaaa simanzi na mateso ya muda mrefu,ilisema “John naumia mume wangu, hali yangu kila kukicha afadhali ya jana”. 

John alijibu “usijali Savannah nipo hapa mke wangu kwa ajili yako utapona tu tutakwenda hospitali,subiri nikuandalie chakula ule, kisha nikupeleke hospitali malikia wangu”. Basi baada ya John kumfariji Savannah aliamka na kuelekea jikoni pembeni ya sehemu aliyokuwa amelala mpenzi wake. 

Watu hawa walipendana sana ni vile tu hali yao haikuwa nzuri kifedha waliishi kwa kuhangaika, kuomba msaada na wakati mwingine walifukuzwa na walimwengu pale walipokuwa wakiomba msaada, watu waliwapita kama mbwa waliokosa matunzo. 

Wapenzi hao Walizoea maisha ya kuokota vyakula jalalani na kukimbilia magari ya taka sambamba na kusubiria mabaki ya chakula katika migahawa mbalimbali. Wakati huo John alikuwa akitimiza ahadi aliyo mhahidi malikia wake alimuandalia chakula walicho kiokota katika soko kuu la mji huo wa Chatu. John alimuinua Savannah pale alipokuwa amelala kwenye kanga chakavu akiwa amejifunika magunia yalionekana ni ya mpunga. John alimlisha Savannah chakula kile ambacho hawakujua kilipikwa lini na kutupwa na nani na lini. Savannah alisikika akisema “asante mume wangu hata 

mwanangu anafurahi sasa naona napata nafuu, nahisi ni njaa ilikuwa inaniuma”. Mwanangu nisamehe mama kakushindisha njaa, nakupenda sana najua wewe utakuwa mrembo zaidi yangu mwanangu hata baba yako anakupenda”. John alikuwa anapenda sana utani alicheka na kusema “atakuwa mrembo kama wewe kweli mke wangu lakini rangi ya ngozi yake itakuwa kama yangu, yako iko kama ya nguruwe hahahaaaa!” Savannah alikuwa mweupe kama Nguruwe, ingawa alivyokuwa anaonekana ni kama mtu mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde kutokana na ugumu wa maisha. 

Wawili hao walifurahi pamoja na kusahau shida walizokuwa nazo.Walipomaliza kula wapenzi hao waliamua kutoka nje baada ya kukaa ndani ya paghala hilo kwa muda wa wiki moja, Dikidiki hao walikuwa na kaida ya kufanya hivyo wanapotafuta riziki na kujilimbikizia ndani ya paghala lao kisha wana kaa kwa muda huo bila kutoka. Usilolijua ni kama usiku wa kiza, basi Savannah na John walipotoka wakiwa n’je ya mgahawa mmoja uliokuwa unapendwa sana na wananchi wa mji huo wa Chatu zilisikika sauti za wanawake wakisema: 

“haya jamani sasa ni ule wakati wa Pesa nyingi kuingiza hela sasa wenzi wametoka fungate”. Waliamini kuwa Pesa nyingi alikuwa anawatumia Dikidiki hao kama misukule inayotoka na kurudi ndani na wanapotoka basi mzee Pesa nyingi huingiza hela nyingi sana. Kwakuwa wenzi hao walikuwa hawaelewi kinachoongelewa waliendelea kuomba msaada kwa wateja waliokuwepo hapo mgahawani. Wanapokosa waliamua kucheza baadhi ya nyimbo zilizokuwa 

zikipigwa katika mgahawa huo, wakicheza hupewa chakula na fedha ambazo hutoka katika mifuko ya wateja. John alikuwa anapenda sana kucheza,wakiwa wamekaa chini walisikia wimbo wa mwanamuziki maarufu Tanzania Diamond unaosema Je, Utanipendaga? John alimuinua Savannah aliyeonekana kachoka na mimba yake. Savannah aliamka na kucheza na mpenzi wake ,walicheza kwa miondoko ya kihindi, machozi yalisafisha uso wa Savannah huku yakiosha kifua cha John kilichokuwa kimejaa kama mlima na mikono iliyokuwa na miinuko ya kupanda na kushuka ilizunguka juu ya kifua cha Savannah na kumfanya ahisi kazungukwa na jeshi kubwa la malaika wa ulinzi.

Baada ya kumaliza kucheza savannah alikuwa amechoka sana, kitendo cha kucheza kilimsababishia kuchokoza maumivu na kupelekea kupata uchungu katika kizazi chake. Baada ya kuona hivyo John aliinama na kuchukua zawadi walizozipata kutoka kwa hadhira iliyokuwa ikiwatazama huku baadhi ya hadhira wakibubujikwa na machozi walimpelekea hela na chakula John katika kapu lake la kukusanyia riziki. Watu waliokuwa wakiwatazama Savannah na John hawakujali maumivu ya mwanamke yule na kuona kawaida. 

Wapo waliosikika wakisema hawa vichaa wana akili, wengine walisema hawa si vichaa, vichaa gani wana akili ya kutafuta hela hivi, wamekusanya umati mkubwa hivi na kuwafanya watu kutoa kile walichonacho. Mama mmoja mwenye busara anayeuza katika mgahawa huo aliyefahamika kwa jina la mama ndaga akasema“Jamani mimi nawafahamu hawa vichaa kwanza hawakuwa wakitembea hivi pamoja kama Dikidiki, huyo kaka unayemuona alikuwa..........pata mwendelezo kwa kujipatia kitabu hiki.


Nicheki kwa mawasiliano haya:+255756377940
Instagram: @sinyatiblog
Facebook:Tupokigwe Abnery 








MJUE BLOGGER TUPOKIGWE ABNERY MWANDISHI WA KITABU CHA RIWAYA "MAPENZI KABURINI" MJUE BLOGGER TUPOKIGWE ABNERY MWANDISHI WA KITABU CHA RIWAYA "MAPENZI KABURINI" Reviewed by Erasto Paul on September 17, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.