Katika
kuwakumbuka wenzao waliopoteza maisha wakati wa harakati za kupigania uhuru wa
nchi, wanajeshi wa Kikosi cha Rada (03/691KJ) wanaolinda mpaka wa Tanzania na
Kenya, wamefanya usafi kwenye Kituo cha Afya cha Oldonyosambu kilichoko jirani
na kambi hiyo.
Kumbukumbu
hiyo imefanyika leo ikiwa ni Siku ya Mashujaa ambayo huadhimishwa Julai 25 ya
kila mwaka ikilenga kuwakumbuka na kuwaenzi wanajeshi waliopoteza maisha wakiwa
kwenye majukumu ya kupigania uhuru wa nchi katika nchi za Afrika.
Akizungumza
wakati wa kufanya usafi, SSGT Kennedy Laizer aliyemwakilisha Mkuu wa kikosi
hicho, Kapteni M.J. Shomari amesema pia wamefanya kazi hiyo kwa ajili ya
kuboresha uhusiano kati yao na wananchi.
Laizer
amesema wamepokea changamoto kutoka kwa wananchi ya ukosefu wa uzio na jengo la
wodi ya wagonjwa, akiahidi kusaidia kuitatua kwa kadri watakavyoweza.
Akizungumzia
changamoto za kituo hicho cha afya, Mganga Mfawidhi, Aziza Saidi amesema
wamekuwa wakipatwa na matatizo mengi kutokana na ukosefu wa uzio, ikiwemo kuvamiwa
na wanyama na mifugo.
“Tumejaribu
kupanda miti katika eneo la kituo lakini mifugo iliiharibu. Usiku tunafanya
kazi kwa wasiwasi wa kuvamiwa hata na majambazi maana hakuna uzio lakini pia
nyumba za wahudumu ni shida, wengi wanatoka mbali hadi wanachelewa kazini,”
amesema.
Saidi
ameiomba Serikali kuwajengea jengo la wodi kwa kuwa moja lililopo limegawanywa
na linatumika kwa ajili ya wanawake na wanaume.
Diwani wa
Oldonyosambu, Raymond Lairumbe amesema kituo hicho walikijenga kutokana na
wananchi kuteseka na huduma za tiba, hivyo kwa walipofikia wanaiomba Serikali
kuwasaidia sehemu iliyobaki.
Wanajeshi wawakumbuka wenzao kwa kufanya usafi
Reviewed by Erasto Paul
on
July 25, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili