Sekondari Idodi yajengewa bweni la Sh 270 milioni


Balozi wa Japan nchini  Tanzania Masaharu

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan, amesaidia ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari Idodi wilayani Iringa.
Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa,  amesema bweni hilo litagharimu Sh 270 milioni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bweni hilo, Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida amesema kuwa misaada hiyo inatolewa kupitia kodi za watu wa Japan kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za kimaendeleo nchini Tanzania.
Ubalozi huo wa Japan ambao umesaidia ujenzi wa bweni la wanafunzi baada ya kuwepo kwa maombi ya Waziri Lukuvi aliyoyaomba katika ofisi ya ubalozi baada ya bweni hilo kuteketea kwa moto.
Balozi huyo amesema kuwa mkataba wa ujenzi wa bweni hilo la wanafunzi ulisainiwa Februari mwaka 2016 kwa dola za kimarekani 130,166 zaidi ya Sh 270 milioni za kitanzania kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo.
Ubalozi wa Japan nchini umeahidi kuendelea kusaidia miradi mbalimbali ya kimaendeleo ndani ya mkoa wa Iringa na maeneo mengine hapa nchini ili kuunga mkono jitihada za Serikali.
"Waziri Lukuvi alileta maombi ya miradi mbalimbali ambayo miongoni mwake ni kujengewa hosteli ya wasichana ya Shule ya Isimani ambayo ilijengwa toka mwaka 2005 na mwaka 2008, kujenga jengo la OPD na wodi ya wagonjwa katika zahanati ya Mlowa na mwaka 2010 kununua gari la wagonjwa katika zahanati ya Mlowa, kwa hiyo namshukuru Waziri Lukuvi kwa kusimamia vema miradi hiyo,"amesema balozi huyo.
"Leo nimefurahi kuona ujenzi umekamilika kwa kiwango kizuri vitanda vya kutosha, mfumo wa kuhifadhi maji wa hosteli hii umekamilika ikiwa na uwezo wa kulaza wanafunzi 208 kama kusudio la ujenzi, na ni matumaini yangu mradi huu utatunzwa vema,"ameongeza.
Balozi huyo amesema kutokana na usimamizi mzuri walioufanya, Kampuni ya Koyo Corporation ya Japan imetoa msaada wa taa zinazotumia nguvu ya mionzi ya jua kwa ajili ya  wanafunzi wote watakaoishi katika bweni hilo.
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza awali akimkaribisha balozi huyo amesema kuwa Serikali ya mkoa inafurahishwa na msaada huo ambao umesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi bwenini.
Waziri Lukuvi pamoja na kupongeza msaada huo wa kujengewa bweni na miradi mingine amewataka wanafunzi hao kutunza mabweni hayo na kujiepusha na hatari zozote za kuchoma moto, kitendo ambacho kinasababisha upotevu mkubwa wa mali na uhai wa wanafunzi hao.
Sekondari Idodi yajengewa bweni la Sh 270 milioni Sekondari Idodi yajengewa bweni la Sh 270 milioni Reviewed by Erasto Paul on July 25, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.