Mwanza. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kuwaua watu sita
wanaodaiwa kuwa majambazi na wengine wawili kukimbia katika Mtaa wa Fumagila
Mashariki Kata ya Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza, taharuki imeendelea
kuwakumba wananchi wa eneo hilo wakihofu kuwa huenda wakarudi.
Akizungumza na gazeti hili leo
Jumapili, Julai 9, Mwenyekiti wa mtaa huo, William Ngemela amesema tukio hilo
limetoa elimu tosha katika mtaa huo na mitaa jirani huku akidai tangu azaliwe
hajawahi kushuhudia tukio kama hilo.
“Hii ni elimu tosha kwasababu haya
yote hatukutegemea kama yanaweza kutokea kwenye mtaa kama huu, lakini angalia
silaha zote na vitu vilivyokamatwa, kwakweli inatishia amani,” amesema Ngemela.
Katika tukio hilo polisi walikamata
silaha ya SMG AK47, magazine mbili kila moja ikiwa na risasi 30, risasi 36 za
AK 47ambazo zilikuwa nje ya magazine, risasi moja aina ya rafal, risasi nane za
shortgun.
Silaha nyingine ni bastola nne za
kienyeji, sare za jeshi za nchi jirani, kofia sita za kuziba uso, kitambaa cha
kichwani, nusu kanzu, nguo mbalimbali za kiume, mabegi matatu yaliyokuwa
yakihifadhi silaha hizo, baiskeli mbili, pikipiki moja, unga na dagaa.
Mwenyekiti huyo amesema watu hao
walikuja mtaani hapo kama waumini wa dini ya kiislamu kumbe walikuwa na mambo
yao, lakini hili limekuwa fundisho kwetu ni wajibu wetu wote kushirikiana, mimi
ni mwenyekiti mmoja lakini jamii ninayoingoza ni kubwa inapaswa kutoa taarifa.”
Amesema tangu lilipotokea tukio hilo
jana, baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawakutoka nje ya nyumba zao walijifungia
wakiogopa kuwa hao waliokimbia wanaweza kurudi kufanya jambo baya, kwahiyo hali
bado haijawa nzuri kwa wakazi wangu.”
Ishmael John, mkazi wa mtaa wa
Kanenwa, alisema, “kiukweli hatuwezi kuwa na amani ya kutosha kutokana na jinsi
hali ilivyokuwa juzi.”
Mkazi mwingine wa mtaa huo, Robert
Musabi amesema itakuwa vigumu kuamini kwamba hali itakuwa salama hususani
ukizingatia baada ya wawili kukimbilia kusikojulikana.
Hata hivyo mwenyekiti wa mtaa wa Kanenwa
jirani na mtaa huo, James Buduma amesema serikali za mitaa eneo hilo tayari
zimeanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella la kusajili
kila mtu ambaye anafika akiwa mgeni na ajitambulishe uhalisia wake.
Kamanada wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Ahmed Msangi amesema zoezi hilo la kuwasaka wahalifu ni endelevu na hakuna
atakayesalimika katika operesheni hiyo hivyo kuwataka wanaofanya vitendo hivyo
waache mara moja.
Vifo vya watu sita vyazua taharuki Mwanza, wananchi wajifungia ndani
Reviewed by Erasto Paul
on
July 09, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili