Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Joel
Malongo, amekishauri Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT)
kusambaza huduma zake katika maeneo mengine ya nchi ili kuongeza elimu na tija
kwa wakulima nchini.
Akizungumza
katika mkutano wa kazi uliolenga kufahamiana baina ya wadau wa masuala ya
kilimo kutoka sekta ya umma na binafsi kilichofanyika Dodoma hivi karibuni,
Mhandisi Malongo amesema:
“Ukanda
huu wa SAGCOT unazalisha asilimia 65 ya chakula cha nchi, maana yake ipo haja
ya kuhamasisha uwekezaji zaidi ili malighafi kama nyanya, viazi na bidhaa za
maziwa zisisafirishwe nje ya nchi zikiwa ghafi.” Amesema na kuongeza;
“Ikiwa
Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini umefanikiwa kufanya maajabu haya katika kilimo, maana
yake maeneo mengine ya nchi yanahitaji kuendelezwa pia kwa ajili ya kufikia
malengo ya Tanzania ya viwanda.”
Mhandisi
Malongo amesema upande wa Mashariki ya nchi kuna uzalishaji wa katani, hiliki
na mazao mengine ya biashara na kusema kuwa hili litasaidia kuangalia uwezekano
wa kuendeleza mazao yasiyo ya chakula.
Mhandisi
Malongo amesema upande wa Kaskazini kuna wazalishaji wazuri wa
pamba.
‘Sasa hivi
nchi za Afrika Mashariki zimepiga marufuku kuingiza mitumba ya nguo na viatu.
Ipo haja kuvijengea uwezo viwanda vyetu vipate pamba nyingi kwa ajili ya mavazi
kwani viwanda vya nguo vinazalisha ajira nyingi. Ile ndoto yetu ya kuwa na
asilimia 40 ya ajira katika viwanda itimie.” Amesema
Naibu
Katibu Mkuu huyo amesema, hali ya hewa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni
nzuri kwa ufugaji hivyo ipo haja ya kutengeneza viwanda vingi kwa ajili ya
mazao ya maziwa na kusisitiza kuongeza viwanda katika maeneo mengi ya nchi.
“Mwezi
uliopita Rais John Magufuli alizindua kiwanda cha matrekta cha Ursus mkoani
Pwani, tumepanga kuyauza kwa bei nafuu ili yawafikie wakulima. Natoa rai kwa
watu wa SAGCOT, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na NDC waangalie namna ya
kusambaza matrekta haya kwa wakulima ili msimu ujao mavuno yaongezeke,” amesema
Mhandisi Malongo.
Naye,
Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga amesema kikao
kimezingatia umuhimu wa kiasi cha bidhaa kinachohitajika. Mfano
kiwanda cha kusindika nyanya kinakosa nyanya za kutosha na matokeo yake
wanaagiza kutoka nje.
“Hii
changamoto lakini pia ni fursa kwa wakulima kuongeza uzalishaji, kutokana na
uwekezaji uliofanyika katika maeneo hayo naomba wakulima wachangamkie.”
Amesema.
Ametoa
mfano wa Kiwanda cha Silver Land kilichopo Iringa kinachozalisha
chakula cha mifugo na kusema kiwanda hicho kinachakata tani 40 kwa saa lakini
hakipati kiasi cha kutosha cha soya na mahindi. Kwa hiyo kinalazimika kuagiza
kutoka nje ya nchi.
Kirenga
amewataka wazawa wanaofanya kazi katika viwanda vya wawekezaji wa nje
watumie fursa hiyo kujifunza ili waanzishe viwanda vyao baadaye.
“Wenye
viwanda wa kesho watatokana na wafanyakazi wanaofanya kwenye viwanda vya
wageni, pale tunapanda mbegu za wenye viwanda wa baadaye. Wanapofanya kazi
wasiangalie mshahara tu bali mafunzo wajiongeze kazi iwe darasa lao, kwa sababu
viwanda vitakavyotengenezwa si lazima viwe vikubwa hata katika mataifa
yaliyoendelea walianza kwa viwanda vidogo lakini leo ndio wenye viwanda
vikubwa,” amesema Kirenga.
Miongoni
mwa wahisani wa shughuli zinazoendeshwa na SAGCOT katika Nyanda za Juu Kusini
ni pamoja na Serikali ya Tanzania, UKAID, USAID, Benki ya Dunia, Ubalozi wa
Norway, UNDP na AGRA.
SAGCOT watakiwa kusambaza huduma ili kuongeza tija
Reviewed by Erasto Paul
on
July 09, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili