TCU yavifutia udahili vyuo 19, yafuta kozi 75



 

Ofisa habari wa TCU, Edward Makaku
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imevifutia udahili vyuo 19 na kufuta kozi 75 katika vyuo 22 kwa kukiuka sheria, taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu nchini.
Ofisa habari wa tume hiyo, Edward Makaku amesema uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza agizo la Serikali lililoitaka tume hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili viweze kutoa elimu bora.
Makaku amesema kuwa kwa vyuo ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo mabadiliko haya hayatawahusu, wanatakiwa kuendelea na masomo kama kawaida, ila vyuo hivyo  haiviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huu wa masomo.
Alizitaja sababu  zilizopelekea baadhi ya vyuo kufutiwa udahili wa shahada, shahada za uzamili pamoja na shahada za uzamivu kuwa ni kukosa vitendeakazi na wataalam katika kufundisha elimu ya juu.
Mkaku pia amesema kwamba TCU imeandaa maonyesho yatakayoanza Julai 26, 2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, pia kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na tume hiyo.
Mkaku pia amesema baadhi ya vyuo vinavyotoa taaluma za afya kama Kilimanjaro Christian Medical College (KCMC) cha mkoani Kilimanjaro, Kampala International University (KIU) cha  Jijini Dar es Salaam na  Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) pia cha Jijini  Dar es Salaam hawakuwa na vifaa na wataalam wa kutosha kufundisha kozi hizo.
Amesema vyuo hivyo vilikuwa vikitoa kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya uzamili katika udaktari wa magonjwa ya kinamama.
Alivitaja vyuo  vilivyofungiwa kutokana na kutokuwa na wataalam wa kutosha kuendesha kozi zake kuwa ni, St. Joseph, St. John, Tumaini University pamoja na vyuo vingine kadhaa ambavyo havina waalimu pamoja na vifaa kwa mujibu wa maelekezo ya tume hiyo.
Mkaku amebainisha kuwa katika vyuo 22 hapa nchini kuna zaidi ya kozi 75 ambazo hazitakiwi kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Amewashauri watahiniwa wanaotarajia kujiunga kwa mwaka huu wa masomo kuingia katika tovuti rasmi za vyuo ili kujua kozi ambazo zinatakiwa na ambazo zimezuiwa.
“Tulifanya uhakiki wa vyuo hapa nchni Septemba na Oktoba 2016 na kubaini baadhi ya vyuo kutokidhi mahitaji ya watahiniwa katika baadhi ya kozi kwa hiyo ni muhimu kutoa taarifa mapema kwa umma juu ya  mchakato huu,” amesema.
TCU yavifutia udahili vyuo 19, yafuta kozi 75 TCU yavifutia udahili vyuo 19, yafuta kozi 75 Reviewed by Erasto Paul on July 25, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.