Rais John
Magufuli ni kama amemuweka katika mtego Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena
Sakaya baada ya kumpongeza kwa ushirikiano wake katika shughuli za maendeleo
huku akisema ingawa kimwili mbunge huyo ni wa CUF, lakini damu yake na roho
yake ni vya CCM.
Rais Magufuli
ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, alisema hayo jana wakati akizungumza na
wananchi wa Kaliua, Tabora wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Kaliua –
Kazilambwa, kwenye Uwanja wa Kasungu.
Barabara
hiyo yenye urefu wa kilomita 56, imejengwa kwa kiwango cha lami kwa zaidi ya
Sh61.86 bilioni, zote zikiwa ni fedha za ndani.
Akimzungumzia
Sakaya ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Rais Magufuli alisema amekuwa
akifanya kazi nzuri za maendeleo katika kutekeleza ilani ya CCM, huku akimtaka
kuendelea kuwapa maendeleo wananchi bila kuwabagua kwa itikadi ya vyama vyao na
akawataka wanaCCM kushirikiana naye. Alisema kuwa ni bora kuwa na wanachama wa
chama kingine anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana-CCM anayefanya kazi
za vyama vingine.
“Mheshimiwa
Sakaya ukimwangalia mwili wake ni mwana-CUF, lakini damu yake na roho yake ni
mwana CCM. Inawezekana siku moja akahamia CCM. Ni bora kuwa na mwanaCUF, au
mwana Chadema, au mwana-ACT anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana CCM
anayefanya kazi za chama kingine. Si mmenielewa? Mimi najua maana hata wakati
wa kampeni niliyaona.”
Awali,
akitoa salaam zake kwa niaba ya wananchi wa Kaliua, Sakaya alimpongeza Rais
Magufuli na kumhakikishia kuwa anamuunga mkono kwa juhudi zake za kuwatetea
Watanzania na kuwaletea maendeleo akisema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa
wananchi wa jimbo lake ambao alisema asilimia 85 ni wakulima.
Pia,
alimuomba awaongezee kilomita nyingine za lami pamoja na huduma ya maji
aliyosema ni tatizo kubwa, ili Kaliua ipige hatua za maendeleo haraka.
Katika
hotuba yake, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuongeza barabara nyingine zenye jumla ya
urefu wa kilomita 112 akisema fedha si tatizo.
Hizo ni
pamoja na barabara ya Kahama - Urambo ya kilomita 28 ambayo mchakato wake wa
ujenzi unaanza ndani ya mwezi na Chanya -Nyaua ya kilomita 84 ambayo nayo
mchakato wake ni ndani ya siku 45.
Pia Rais
Magufuli ameziagiza mamlaka zinazohusika na ujenzi wa reli ya kisasa, kuanza
kubomoa nyumba za wanaCCM waliojenga kwenye hifadhi ya reli hiyo zao huku
akisema kuwa sheria ni msumeno.
Aliwataka
pia waliojenga kandokando ya reli hiyo kujiandaa kisaikolojia kwa kuwa zote
zitaondolewa. “Kuna baadhi ya watu tena wengine ni wanaCCM wanaopitapita na
kusema kuwa hazitabomolewa, ukifika wakati anzeni na za wana-CCM. Mimi ndio
mwenyekiti wa CCM, lakini sheria ni msumeno,” alisema.
Kuhusu
mazingira, Rais Magufuli alisema Mkoa wa Tabora ulikuwa na sifa ya kuyahifadhi
lakini sasa nao umeanza kuingiliwa na ugonjwa ulioikumba mikoa mingine wa
kufyeka miti na misitu ovyo.
Alisema
wanaofanya uharibifu huo ni watu kutoka mikoa mingine na kwamba wengine
walikaribishwa na kuruhusiwa na baadhi ya wana CCM kukaa kwenye maeneo ya
hifadhi na kuwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini
kote kusimamia sheria katika kulinda mazingira na maeneo ya hifadhi.
Sakaya awekwa mtegoni CCM, CUF.
Reviewed by Erasto Paul
on
July 24, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili