Aliyeitwa tumbili, amegeuka kuwa shujaa.



Aliyeitwa tumbili, amegeuka kuwa shujaa.
Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais John Magufuli kummwagia sifa mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila kwa kuibua na kulivalia njuga sakata la uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Magufuli alimwaga sifa hizo jana mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wake wa hadhara katika vijiji vya Uvinza na Nguruka wilayani Uvinza, Kigoma ambako alizindua mradi wa maji uliogharimu Sh2 bilioni.
Mradi huo utahudumia vijiji vya Nguruka, Bweru, Nyangabo, Itebula na Kasisi.
“Lazima niwe mkweli na nisiposema hapa nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu,” alisema Rais ambaye yuko katika ziara ya mikoa ya Magharibi.
“Siku zote ukweli utabaki kuwa ukweli tu na ndio maana nampongeza Kafulila kwa sababu alisimama imara kupigania masilahi ya umma. Alionyesha uzalendo wa hali ya juu unaopaswa kuigwa na kila mmoja wetu.”
Magufuli alisema waliomuita Kafulila kuwa ni tumbili, wao ndio wamegeuka kuwa tumbili.
Rais alimtaja Kafulila wakati alipokuwa akizungumzia umuhimu wa wananchi kuwa na uzalendo katika ulinzi wa rasilimali za nchi ambazo zimekuwa zikiibwa na magenge ya wahalifu.
Rais alitoa mfano wa namna Kafulila alivyokubali kutumia nguvu zake zote kupambana na mafisadi waliochota fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, kiasi cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Jaji Frederick Werema kupandwa na hasira na kumfananisha na mnyama huyo wa mwituni.
Kafulila, ambaye alikuwa mbunge wa Kigoma Kusini kuanzia 2010 hadi 2015 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, aliibua kashfa hiyo bungeni baada ya kuisoma katika gazeti la The Citizen mwaka 2014.
Katika sakata hilo, Sh306 bilioni zilichotwa kutoka akaunti hiyo iliyofunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL baada ya kutokubaliana katika tozo ya uwekezaji.
Bunge liliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi na taarifa yake ilitumiwa na chombo hicho cha kuisimamia Serikali kujadili kwa kina uchotwaji huo.
Pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM kuungana na upinzani katika sakata hilo, mijadala ilitawaliwa na mihemko na ushabiki na haikuwa ajabu kwa Werema kujikuta akitoa kauli hiyo.
Siku ya tukio, Kafulila aliomba mwongozo wa Serikali kuhusu fedha hizo akisema Jaji Werema alisema uongo kuwa waliruhusu zitolewe kwa kutii amri ya Mahakama.
“Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda kinyume,” alisema Kafulila.
Baada ya maelezo ya mwongozo wake, Jaji Werema alijibu kwa kueleza historia ya mgogoro wa Tanesco na IPTL na fedha za escrow, huku Kafulila na mbunge wa Kibamba, John Mnyika wakitaka kusimama kila mara kuomba mwongozo wa kupinga maelezo yake.
Hali hiyo ilimkasirisha Jaji Werema kiasi cha kushindwa kujizuia.
“Wanyankole wanasema tumbili hawezi kuamua masuala ya misituni. Sikiliza tumbili, sikiliza please (tafadhali),” alisema Jaji Werema huku Bunge likilipuka kelele kutoka upande wa upinzani.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge siku hiyo, Hassan Zungu alizuia vurumai hizo kwa kumtaka Jaji Werema kukaa na kisha kuwataka wabunge hao wawili kupeleka ushahidi wao Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru).
Mara baada ya kikao kuahirishwa, Jaji Werema ambaye awali alikuwa amesema, “Kama unataka kuleta mambo ya nje, ndani ya Bunge ningojee pale nje,” alisimama na kuonekana anataka kwenda sehemu alikokuwa Kafulila, lakini kabla hajamfikia, mawaziri walimzuia na kwenda naye nje ya ukumbi.
Sakata hilo la escrow bungeni lilisababisha Jaji Werema kujiuzulu na kufuatiwa na Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Pia, wenyeviti watatu wa kamati za Bunge, Andrew Chenge, William Ngeleja, ambao walipewa fedha zilizoonekana kutoka kwenye akaunti hiyo, na Victor Mwambalaswa, walivuliwa nyadhifa zao.
Sakata hilo lilionekana kama limeisha licha ya baadhi ya maazimio ya Bunge kutotekelezwa, lakini Juni 19, watuhumiwa wakuu katika kashfa ya escrow, Harbinder Singh Seth na James Rugemalira walifikishwa mahakamani na Takukuru na kusomewa mashtaka tofauti, ikiwa ni pamoja na uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Seth ni mmiliki wa kampuni ya Pan African Power Solution (PAP), ambayo ilichotewa fedha hizo kutokana na kuonyesha kuwa imeinunua IPTL, wakati Rugemalira ni mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL.
Wakati sakata hilo likiwa mahakamani, Julai 9, Ngeleja ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, alitangaza kurejesha serikalini Sh40.4 bilioni za mgawo wa escrow.
Alitumia akaunti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuzirejesha lakini chombo hicho kimezikataa fedha hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola ameshawaonya kuwa wote waliopokea fedha hizo kuwa hawako salama na kwamba taasisi yake inaendelea na uchunguzi.
Kafulila anena
Kafulila, ambaye alitangaza kuihama NCCR-Mageuzi na kujiunga na Chadema kwa maelezo ya kutaka kuunganisha nguvu, alifurahia kauli hiyo ya Rais Magufuli kuhusu hatua alizochukua kuibua kashfa ya escrow.
“Nimefarijika kuona mkuu wa nchi ameguswa na kutambua mchango wangu katika vita hatari ya ufisadi wa IPTL/Escrow,” amesema Kafulila katika ujumbe alioitumia Mwananchi jana.
“Kwenye vita hii hakuna chama. Niliteseka sana ndani na nje ya jimbo kutokana na vita hii. Zilifanyika kila hila na njama lakini namshukuru Mungu kuwa upande wangu nimebaki hai.
“Ukweli nimefarijika sana kuona mkuu wa nchi amelizungumzia jambo hili jimboni kwa wananchi walionipenda sana.”
Kingine kilichomfurahisha Kafulila ni jinsi Rais alivyozungumzia suala hilo, “Amezungumzia kwa hisia na uzito wa kutosha, jambo lililonifariji zaidi.
“Binafsi kwenye vita ya ufisadi nchini ninamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Ushauri wangu ajenge mfumo na taasisi imara za uchunguzi na uendeshaji mashtaka katika eneo hili ili kuhakikisha vita hii inakuwa ya mafanikio makubwa,” alisema.
Alisema anatamani kuona hakuna jiwe linalosalia katika ufisadi uliofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwamo waliobeba mabilioni kwa lumbesa kutoka benki ya Stanbic ambao tofauti na wenzao, hawajawahi kutajwa hadharani.
Aliyeitwa tumbili, amegeuka kuwa shujaa. Aliyeitwa tumbili, amegeuka kuwa shujaa. Reviewed by Erasto Paul on July 24, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.