By Dk Shita Samwe
Leo tunageukia matatizo ya kisaikologia yanavyoweza
kuathiri nguvu za kiume.
Kama nilivyowahi kueleza hapo awali kuwa tendo la ndoa
linahusisha mtiririko wa matukio mengi ya kimwili, huku ubongo ndio mhimili
mkuu wa jambo hilo kuweza kutendeka.
Ubongo ndio unaopokea na kutafsiri mambo ya kimwili
ikiwamo hisia za kimwili na kufanya uamuzi wa nini kifanyike.
Na ili uweze kufanya matukio haya, kuna hitajika kusiwe
na mwingiliano wa shughuli za mfumo wa fahamu.
Matatizo ya kisaikologia yanachangia tatizo la nguvu za
kiume kwa kati ya asilimia 10-20. Huwa ni matokeo baada ya kuwapo kwa chanzo
kingine, mfano unaweza ukajikuta umefukuzwa kazi hivyo ukawa una mawazo mazito.
Mawazo hayo yanakufanya usiwe na utulivu wakiakili hali inayoathiri hisia
zako.
Mara nyingi matatizo yakisaikologia yanaweza kuanza
nyakati za utotoni baada ya kunyanyaswa kijinsia au kuumizwa kimapenzi.
Matatizo hayo ambayo yanajitokeza katika jamii yetu ni
pamoja na kupewa malezi mabaya, kufanyiwa vitendo viovu, mifarakano ya wazazi,
kulawitiwa na kuona matukio ya kutisha utotoni.
Ukiacha hayo, yapo matatizo yakisaikologia ambayo ndio
mara nyingi huchangia uwapo wa tatizo hili ikiwamo haya yafuatayo;
Shinikizo la kiakili (stress) ni tatizo ambalo lipo katika jamii na linaweza
kumuathiri mtu ikiwamo matatizo ya kazini, kifedha, mifarakano ya ndoa/mapenzi
na maudhi mbalimbali.
Pale mwanaume yeyote anapojikuta amepata tatizo hili kwa
mara ya kwanza, hujikuta ana kuwa mwoga na mwenye wasiwasi pale anapokutana na
mtu kwa mara nyingine.
Huwa anakuwa amejenga dhana akilini mwake kuwa huenda
atashindwa tena na kuabika kwa mwenza wake. Mwanaume huyo hujikuta akijihisi
kuwa yeye ni mkosaji kwa kushindwa kumridhisha mwenza wake.
Sonona/mfadhaiko wa kiakili ni tatizo linalowakuta
wanaume ambao hujikuta wakiathiri nguvu zao za kiume. Uwapo wa tatizo hili
humuathiri mtu kiakili na kimaumbile.
Pia, linaweza kumuathiri hata akiwa amepata utulivu wa
kuweza kujamiana na mwenza wake.
Kutojiamini kwa mtu ni chanzo kingine cha kushindwa kuwa
na nguvu za kiume, kujiona kuwa hamtoshelezi mwenza wake.
Kujiona ukotofauti; huwapata watu wenye umri mkubwa
wakiwamo wazee kabisa. Kwani umri unaposogea, mtu hukosa mwamko wa kuhitaji
tendo la ndoa.
Hujaribu kukumbuka kipindi akiwa kijana na mwenye nguvu
zilizomfanya aweze kutenda tendo hilo kiufasaha. Sasa wanapo kuwa wazee
hujikatia tamaa na kujiona wadhaifu na hapo ndipo huweza kujiathiri zaidi na
zaidi.
Mara nyingine watu wenye umri mkubwa huwa na matatizo
mbalimbali ya kiafya yanayochangia kudhoofika mwili na hasa kukiwa na
mifarakano inayoweza kusababisha vurugu kwenye uhusiano.
Mtu anaweza akawa amefiwa na mkewe, hujikuta akipata hali
ya simanzi kwa muda mrefu. Hali hiyo nayo inaweza kumsababishia kukosa mwamko
wa tendo.
Usikose toleo lako wiki ijayo kwani tumefikia hatua
muhimu ya uchunguzi na matibabu ya kupungua/kukosa nguvu za kiume.
MWANANCHI
Saikolojia inavyoathiri nguvu za kiume.
Reviewed by Erasto Paul
on
July 07, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili