Baada ya kuona makala mbalimbali zimekuwa zikizungumzia
sababu zinazochangia matatizo ya nguvu za kiume, sasa ungana nami kusoma
kipengele muhimu kinachohusu suluhisho la matatizo ya nguvu za kiume.
Kikubwa unachotakiwa kufanya ili kuweza kupata msaada wa
tatizo hilo ni kuwa tayari kuweka wazi tatizo lako kwa watoa huduma za afya wa
tiba za binadamu na sio kwa watoa huduma wasiotambulika. Hata kama ikitokea
tatizo lako linaweza lisitatulike, ni vizuri ukakubaliana na hali hiyo, tambua
kuwa kukosa nguvu za kiume si mwisho wa maisha yako.
Uwapo wa matangazo mengi mtaani ya dawa za kuongeza nguvu
za kiume haumanishi kuwa yanaweza kutatua tatizo lako, hiyo ni biashara ya wajanja
wa mataani. Unaweza ukawa unatumia dawa hizo na kupata nafuu na ukadhani
kuwa umepona, lakini kumbe ukawa unaudhuru zaidi mwili wako bila kujua.
Dawa hizo hazijathibitishwa wala kupendekezwa kama
ni salama na Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA), yapo kila mahali mitaani
na wengi hujikuta wakinunua na kuyatumia kiholela.
Tayari imeshawahi kuripotiwa kuna watu wamepoteza maisha
baada ya kunywa dawa hizo kiholela pasipo kuzingatia ushauri wa wataalamu wa
tiba.
Tatizo la nguvu za kiume linaweza kutibiwa au
likapunguzwa makali kwa matibabu mbalimbali baada ya kufanyiwa uchunguzi na
wataalamu wa afya.
Yapo matatizo ya nguvu za kiume ambayo hayatatuliki kwa
njia yoyote, hivyo mtu mwenye tatizo hilo huwa ni ulemavu wa kudumu.
Kabla ya kufika huko, ni vizuri ukatambua kuwa yapo
matibabu salama unayoweza kuyafanya kuimarisha hali ya tendo kabla ya kumfikia
daktari.
Mazoezi ni moja ya kitu muhimu kwa mtu mwenye
tatizo hilo, kwani humsaidia kuwa imara.
Yawezekana amekua mtu mzima lakini akifanya mazoezi
mepesi ya kutembea yanaweza kumsaidia.
Lakini unene pia ni chanzo kingine cha kupata maradhi
kama kisukari, magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na shinikizo la damu. Maradhi
haya ndio yanayoharibu mishipa ya damu na mishipa ya fahamu na ndio chanzo
kikuu cha kupungukiwa kwa nguvu za kiume.
Aina ya vyakula
Vyakula vya nafaka ambavyo vimesheheni nishati nyingi,
nafaka zenye nyuzinyuzi (fibre) na sukari (complex sugar), husaidia kutunza
uzito wa mwili.
Nafaka husaidia kuzalisha homoni za testosterone kwenye
damu na huwezesha mtu kuwa na nguvu hatimaye kuongeza nguvu zake za kiume.
Kula nafaka zisizokobolewa kama vile brown bread badala
ya white bread, pia
kula nafaka halisi badala ya cornflakes ni jambo zuri kiafya. Zina saidia kutokuupa mwili
mafuta mengi. Ikumbukwe kuwa uwapo wa mafuta mabaya mwilini huharibu mishipa ya
damu ikiwamo ya uume.
Tangawizi ni aina ya kiungo ambacho mizizi yake husisimua
mfumo wa mzunguko wa damu mwilini. Mzunguko unapokuwa mzuri huwezesha damu
kwenda sehemu za viungo vya uzazi bila tatizo.
Tangawizi hutumika sana maeneo ya Asia kwa ajili ya
wanaume wenye tatizo la nguvu za kiume.
Viungo ambavyo viko katika pilau ni mojawapo ya vitu
ambavyo miaka na miaka vimetumika katika maeneo ya Asia na Amerika Kaskazini
kama vyakula vinavyoimarisha nguvu za kiume.
Vyakula vinginevyo.
Pemigranate ni
aina fulani ya matunda yenye rangi nyekundu yenye mwonekano kama apple.
Tunda hili husaidia kuamsha mishipa ya fahamu na kuweka
mawasiliano sahihi ya mwili, hivyo kumuongezea mtu uwezo wa kufanya tendo la
ndoa kwa hamasa kubwa. Humfanya mtumiaji kupokea hisia za mapenzi kwa urahisi
zaidi.
Mvinyo mwekundu unatajwa pia kuwa na uwezo wa
kuuchangamsha mwili na kuongeza msukumo wa damu huku ikimuondolea mtu uchovu
kabla na baada ya tendo la ndoa.
Hii ndio sababu kubwa inayofanya iwekwe vyumbani katika
mahoteli makubwa duniani. Nchi kama Italia, mvinyo ni kinywaji ambacho
hakikosekani mezani kutokana na kuaminika miaka kwa miaka.
Unywaji wa kiasi unaweza kuwa na faida kubwa kwa
kuchochea na kuamsha hisia na kuweza kwenda mizunguko kadhaa.
Mchanganyiko wa mbegu mbalimbali za matunda ikiwamo
tikiti maji, mbegu za maboga pia husaidia kuondoa ACID mwilini na
kumfanya mtu ajione ni mwenye afya njema.
Vanila husaidia kuamsha hamasa mwilini, vanila ni aina ya
kirurubisho ambacho huwa ndani ya vyakula kama ice cream.
Asali, ina madini yanayoitwa boron ambayo husaidia mwili
kutumia homoni.
Hata vitabu vya dini hueleza ulaji wa asali na masega
yake kama mlo wenye kuupa mwili nguvu. Zipo tafiti lukuki kuhusu faida za asali
ikiwamo ya kuongeza nguvu za kiume.
Karanga huhusika moja kwa moja na kutunza mfumo wa
mzunguko wa damu kuwa na afya. Husaidia kuimarisha mzunguko wa damu katika
maeneo ya uzazi, hivyo, kuongeza msisimko wa tendo.
Pia, karanga zina madini muhimu kama ya magineziamu ,
tindikali ya foliki na madini ya zinki ambayo ni muhimu sana katika uzalishaji
wa mbegu za mwanaume na kuongeza hisia. Ulaji wa Chokoleti pia huongeza
uchangamfu mwilini unaomuwezesha mtu anayeshiriki tendo la ndoa kuwa na mguso
sahihi kwenye fikra zake.
Imeandaliwa na Hadija Jumanne;Mwananchi
Pilipili manga, mdalasini vyaweza kusaidia kuokoa ndoa
Reviewed by Erasto Paul
on
July 07, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili