Mke wa Rais, Janeth Magufuli amekutana na wazee wasiojiweza wilayani Chato na kutoa misaada ya vyakula ili kuwapunguzia changamoto zinazowakabili.
Janeth amekabidhi msaada huo leo (Julai 7) kwa wazee
zaidi ya 400 kutoka kata 23 za Wilaya ya Chato mkoani Geita.
Taarifa ya Ikulu imemkariri Janeth akiitaka jamii, watu
binafsi, wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali kushirikiana kuwasaidia wazee
nchini.
Amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wazee hao
kuwa ni chakula, dawa na hata upendo na kuthaminiwa.
“Tunawaomba mnaokaa na wazee muonyeshe upendo, muwasaidie
pale wanapohitaji msaada, kama wewe una nguvu basi msaidie hata kuchota maji na
kukata kuni kwa kuwa hizo ndiyo baraka zenyewe,” amesema.
Wazee hao wamemshukuru mke wa Rais kwa moyo wa kujitolea
na hasa katika kuwasaidia wazee na wasiojiweza.
Wameiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza
changamoto zinazowakabili wazee.
Akisoma risala kwa niaba ya wazee hao, Ofisa Maendeleo wa
Jamii, Lidiana Kasheku ameeleza namna halmashauri ilivyojipanga kutatua
kero za wazee hao ikiwa ni pamoja na kuanzisha baraza la wazee litakalosaidia
kubaini changamoto na aina ya msaada wanaouhitaji.
Amesema pia wamejipanga kutoa kipaumbele kwa wazee katika
huduma mbalimbali ikiwemo matibabu.
Msaada uliokabidhiwa ni mchele, unga wa mahindi, mafuta
ya chakula, sabuni na maharage.
Wilaya ya Chato ina vijiji 115 vyenye wazee zaidi ya
18,000.
Mke wa Rais Magufuli asaidia wazee Chato
Reviewed by Erasto Paul
on
July 07, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili