Mshambuliaji mpya wa Everton,
Wayne Rooney amekuwa kivutio wakati msafara wa timu hiyo ulipowasili jijini Dar
es Salaam leo asubuhi.
Everton iliyowasili kwenye uwanja wa
Ndege wa Kimataifa (JNIA) ilipokelewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na
Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Ndege binafsi ya Everton iliwasili
JNIA saa 2:39 Asubuhi, kabla ya wachezaji kuanza kuingia kwenye basi lao
maalumu huku wakipitia kwa Waziri Mwakyembe na kumpa mkono kuanzia saa 2:55.
Wakati wachezaji wa Everton wakiingia
kwenye basi, mashabiki waliokuwa nyuma ya geti la kuingilia VIP kila mmoja
alionyesha shauku ya kumuona mubashara 'live' Rooney ambaye kana kwamba msafara
huo ulilitambua hilo na Rooney kuwa wa mwisho kushuka.
Aliposhuka Rooney alikwenda kumpa
mkono Waziri Mwakyembe na kisha kuelekea kwenye basi maalumu la timu hiyo,
wakati akielekea kwenye basi baadhi ya mashabiki wake waliokuwa uwanjani hapo
walianza kupaza sauti wengine wakitaka ageuke asimame na kupunga mkono, lakini
wala hakuwa na habari nao zaidi ya kwenda moja kwa moja kwenye basi.
"Jamani hii timu ndiyo
imewasili, ni timu kubwa na Tanzania tunafarijika kwa ujio huu, niwambie tu
Watanzania hata nyinyi Waandishi wa Habari, ulinzi umeimarishwa na katika
mazoezi yao hata ruhusiwa mtu yoyote asiyehusika kwenda.
"Watu wakae nyumbani watulie
wasubiri siku ya mechi (kesho) waende uwanjani kushuhudia," alisema Waziri
Mwakyembe mara baada ya msafara wa Everton kuingia kwenye magari tayari kwa
safari ya kuelekea Hotelini saa 3:10 asubuhi.
Everton itacheza mechi ya kirafiki ya
kimataifa kesho kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya Gor Mahia ya
Kenya.
Rooney aiteka Dar
Reviewed by Erasto Paul
on
July 12, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili