Watoto
mapacha walioungana, Maria na Consolata ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya
Sekondari Udzungwa kwa sasa wanajipanga kuendelea na masomo ya chuo kikuu.
Mapacha hao wamefanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotoka
juzi. Picha ya Maktaba.
Pacha
walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti wamefanya maajabu mengine baada ya
kufaulu mitihani yao ya kidato cha sita kwa kupata matokeo sawa ya Daraja la
Pili.
Pacha hao
wenye ndoto za kuwa walimu walifanana kwenye matokeo ya darasa la saba
walipohitimu katika Shule ya Msingi Ikonda wilayani Makete kwa kupata alama
sawa.
Hata
hivyo, wakiwa Shule ya Sekondari ya Maria Konsolata wilayani Kilolo, Iringa
walitofautiana kwenye ufaulu wa kila somo kwenye matokeo ya kidato cha nne.
Na safari
hii watu wengi walikuwa wakisubiri kusikia matokeo ya pacha hao ambao miezi
kadhaa iliyopita walikuwa gumzo nje na ndani ya nchi baada ya kuhitimu kidato
cha sita.
Wakizungumzia
matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la
Tanzania (Necta), Maria na Consolata walimweleza mwandishi wetu kuwa
wameyapokea kwa furaha kwa kuwa yanawapa nafasi ya kuendelea na masomo ya chuo
kikuu.
Wamesema
wameyapokea vizuri na hawajui wampe nini Mungu.
Pacha hao
wamesema wanatamani kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha
Ruaha (Rucu) ili iwe rahisi kwao kuendelea kulelewa na walezi wao, Shirika la
Masista la Maria Consolata.
Pacha hao
wamehitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Udzungwa na mwalimu mkuu
wa shule hiyo, Edward Fue amesema kufaulu kwao kunaiongezea heshima nyingine ya
kipekee shule hiyo.
“Japo
shule yetu ina mwanafunzi mmoja aliyepata sifuri, kwa kweli matokeo ya watoto
hawa yameisuuza mioyo yetu. Hakika tuna furaha isiyo kifani kwa sababu kila
mmoja hapa shuleni alikuwa akiwaombea kwa dini yake ili wafaulu. Maria na
Consolata wameonyesha mfano mzuri,” amesema.
Mwalimu
Fue alisema shule hiyo ilijitahidi kuwaandalia mazingira mazuri ili kuhakikisha
ndoto yao kielimu inatimia, jambo ambalo limefanikiwa.
Katika
matokeo hayo, Udzungwa ilikuwa na wahitimu 76 na watatu wamepata daraja la
kwanza, 36 daraja la pili wakiwamo Maria na Consolata, 31 daraja la tatu, wanne
daraja la nne na mmoja amepata ziro.
Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati amesema kufaulu kwa mabinti hao ni
fundisho kwa watoto wa kike na watu wote wenye ulemavu nchini.
“Nawafahamu
Maria na Consolata, ni wasichana wanaojituma, hivyo kufaulu ilikuwa haki yao.
Hili liwe funzo kwa watu wengine wenye ulemavu kwamba, wanaweza kufanya maajabu
wakiamua,” amesema Kabati.
Pacha walioungana wapata maajabu matokeo kidato cha sita
Reviewed by Erasto Paul
on
July 17, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili