Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson amewataka wabunge wa viti maalum kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wakipigiwa kura badala ya kuwatelekeza kwa kisingizio cha kutokuwa na majimbo.
Akiendesha
harambee ya kuendeleza mfuko wa uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake ambao ni
wana-CCM wa mkoa wa Songwe ulioanzishwa na Mbunge wa Viti Maalumu,
Juliana Shonza, Naibu Spika alisema zimepatikana Sh35 milioni.
Katika
harambee hiyo, Shonza alitoa Sh20 milioni ikiwa ni ahadi ya kuwapatia mtaji wa
Sh200,000 kila kikundi cha wanawake hao ambao wameanzisha mradi wa ujasiriamali
huku wadau waliofika kuunga mkono jitihada za mbunge huyo kuwainua wanawake wa
mkoa wakichangia Sh15 milioni.
Dk. Tulia
amesema wapo wabunge ambao hawatekelezi kwa vitendo waliyoahidi wananchi wao
kwenye eneo husika na kibaya zaidi akijitokeza mtu mwingine na kutekeleza
yaliyoahidiwa wakati wa kampeni, mbunge wa eneo hilo hukasirika.
“Shonza
asante sana kwa somo hili na kwa kiasi hiki cha Sh35 milioni kila kikundi
kitapata Sh320,000 badala ya Sh200,000 ulizoahidi. Hivyo basi niwaombe
sana wabunge hasa wa CCM kuiga mfano mzuri wa hiki tunachoshuhudia leo hii
kutoka kwa Mbunge Shonza kwa kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa
kupigiwa kura lakini pia kwa kutekeleza ilani ya CCM,” amesema Dk. Tulia.
Shonza
(CCM) amesema baada ya kupewa ridhaa kuwa mbunge, alianza kukutana
na wanawake wa mkoa huo kwa ajili ya kuwahamasisha kujiunga katika
vikundi vya kiujasiriamali na alivisimamia hadi vikapata usajili na
kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kuanzisha mradi wowote utakaowawezesha
kujikopesha wenyewe.
“Mkoa
mzima una kata 100 na kila kata ina kikundi nilichokianzisha na vikundi hivi
kupata usajili ambao niliusimamia mimi niliwaahidi kuwapatia mtaji
wa Sh200,000 kwa kila kikundi waweze kuanzisha mradi wowote wa
ujasiriamali na vingine nashukuru vimeanza kazi za ujasiriamali na vinafanya
kazi, lakini nikaona niwashirikishe wabunge wenzangu wa maeneo mengine na wadau
wengine watakaoniunga mkono kwenye hili na nashukuru mmeonesha ukweli wenu”.
Alisema
wanawake wa Songwe hawahitaji kutafutiwa kazi maofisini ama shughuli ya
kufanya, kwani ni wachapakazi lakini changamoto waliyo nayo ni
mitaji tu kwani uwezo wa kuingia shamba na kuanzisha mradi wowote wa
kiujasiriamali wanao.
Katika
uzinduzi, huo, Mbunge Shonza aliungwa mkono na wabunge mbalimbali akiwamo
Mbunge wa Jimbo la Mtama, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’, Mbunge wa Jimbo la
Pangani Tanga, Jumaa Awesu, Janeth Mbene wa Ileje na Josephat Hasunga wa wa
Jimbo la Vwawa Mbozi.
Mbunge
wa Jimbo la Mtama, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ ambaye alikuwa
mshereheshaji ‘MC’ wa shughuli hiyo, aliwaambia wana-CCM kwamba kitendo
cha kujenga dhana ya kupata mbunge mpya kwa kila kipindi kinasababisha
kila mbunge anayeingia madarakani kuwa na mashaka hivyo kuamua kuitumia
nafasi hiyo kujijenga mwenyewe na familia yake na kuwasahau wapiga kura kwani
anakuwa hana uhakika wa kuendelea kuchaguliwa.
Amesema:
“Wabunge hawa mnaowaona hapa wanahitaji malezi kutoka kwenu wana-CCM na malezi
yenyewe ni kuungwa mkono ili aweze kuwatumikia zaidi nyinyi badala ya
kujinufaisha yeye kwani anakuwa na uhakika zaidi, ngoja niwaambie mimi ni
mbunge kwa kipindi cha pili na kipindi cha tatu nitakuwa mimi kwa sababu
ninaungwa mkono na wananchi.”
Mbunge wa
Jimbo la Ileje Mkoa wa Songwe, Janneth Mbene aliwataka wanawake hao kuhakikisha
fedha hizo wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa pindi wanapokopa huku
wakikumbuka kurejesha mikono kwa ajili ya kuendeleza miradi yao.
Naibu Spika awataka wabunge watimize ahadi kwa wananchi
Reviewed by Erasto Paul
on
July 16, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili