Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia
watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Mahona Pondamali (50) mkazi wa Wilaya ya
Sikonge yanayosadikiwa kufanyika Aprili mwaka huu.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo, Ijumaa, Julai 7, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,
Wilbroad Mtafungwa amesema Aprili 4 mwaka huu, mke wa marehemu Pondamali alitoa
taarifa Polisi za kupotea kwa mume wake katika mazingira ya kutatanisha na
ndipo Jeshi la Polisi lilipoamua kuanza uchunguzi wa tukio hilo na kufanikiwa
kubaini kuwa mtu huyo hakupotea bali aliuawa.
RPC Mtafungwa
amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alikuwa na tabia ya
ulevi na baada ya kulewa alikuwa akimpiga mke wake na watoto.
“Inadaiwa
wanafamilia hiyo waliandaa mpango wa kumkodi mtu wa kumpiga kwa ajili ya
kumrekebisha tabia hali iliyosababisha mauti yake,” amesema.
Amesema kuwa
baada ya wahusika kubaini kuwa amekufa ndipo walipoamua kwenda kumtupa katika
shimo la wachanaji mbao.
“Polisi kwa
kushirikiana na wananchi waligundua kuwa kuna mwili katika shimo la
wachana mbao na kuamua kulifukua ndipo ndugu wa marehemu waliposema
kuwa ni ndugu yao aliyedaiwa kupotea,” amesema.
Amewataja
wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo kuwa ni mke wa marehemu Tatu Said (30),
mtoto wa marehemu Katambi Mahona (13) na mlinzi jamii wa kukodi, Mwanza Mburuka
(31).
Kamanda
Mtafungwa amesema Polisi walifanikiwa kukamata ng’ombe mmoja kwa Mburuka ambaye
inadaiwa kuwa alikuwa ni ujira kwa muuaji, (Mburuka.)
Watuhumiwa
wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Mke, mtoto watuhumiwa kushiriki kumuua baba
Reviewed by Erasto Paul
on
July 07, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili