Masamaki, wenzake waachiwa huru kesi ya uhujumu uchumi



 
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni.
Washtakiwa wameachiwa huru leo Alhamisi (Julai 13) na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali  Mkuu, Timon Vitalis kuiomba Mahakama iwaachie chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.
Wengine walioachiwa huru ni Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru TRA, Habib Mponezya (45), Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton  Mponezya (51), Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi  Mrema (31) na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan (59).
Hata hivyo, baada ya kesi kufutiwa mashtaka na kuachiwa huru, wenzao ambao ni Mchambuzi  Mwandamizi  wa Masuala ya Biashara TRA,  Hamis Omary (48), Meneja wa Operesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Louis (39)  na Haroun Mpande (28) wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA wamesomewa  mashtaka mapya 110.
Pamoja nao kuna washtakiwa wengine wawili.
Masamaki na wenzake walikuwa wakidaiwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya Serikali  kuhusu Sh12.7 bilioni.
Walidaiwa kudanganya kuwa makontena 329 yaliyokuwapo katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kulipwa wakati wakijua si kweli.
Pia, walidaiwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam,  kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh12.7 bilioni.
Masamaki, wenzake waachiwa huru kesi ya uhujumu uchumi Masamaki, wenzake waachiwa huru kesi ya uhujumu uchumi Reviewed by Erasto Paul on July 13, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.