Siku chache
baada ya Chama cha Wafanyabiashara wa Gesi ya Kupikia (LPG) Tanzania
kulalamikia uamuzi wa Kenya kuwafungia kuuza bidhaa hiyo nchini humo,
mazungumzo yamefanyika na zuio hilo kuondolewa.
Mazungumzo
hayo yamefanyika baada ya uhusiano wa kibiashara baina nchi hizo kuonyesha
dalili ya kuzorota kwa siku za karibuni na kusababisha kuzuiwa kwa baadhi ya
bidhaa kusafirishwa katika mataifa haya jirani.
Taarifa
zilizoripotiwa jana na gazeti la Daily Nation la Kenya zilimnukuu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga
akisema mambo yapo sawa.
“Mazungumzo
ya Rais John Magufuli na Uhuru Kenyatta yameleta matokeo chanya,” alikaririwa
Balozi Mahiga.
Kutokana
na makubaliano ya wakuu hao, Kenya sasa itaruhusu uingizaji wa unga wa ngano na
gesi iliyokuwa imezuiwa huku Tanzania ikitoa fursa kwa matairi ya magari,
maziwa na sigara kuingia nchini.
Licha ya
hayo, kamati ya kushughulikia kero mbalimbali za kibiashara baina ya mataifa
haya imeundwa ili kuyapatia ufumbuzi.
Julai 19,
chama cha wafanyabishara wa gesi (Tanzania LPG Association), kilitoa taarifa
kulalamikia zuio la Kenya kuingiza bidhaa hiyo kwa barabara na kuzitaka
serikali husika kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo.
Taarifa
hiyo iliyotolewa na wajumbe watatu; Mohamed Mohammed, Rajesh Chidambaram na
Hamisi Ramadhan imesema marufuku hiyo ingeleta athari kwenye mtaji waliowekeza
kwa kuzingatia kuwa Kenya hununua tani 40,000 za ujazo za gesi hiyo kati ya
tani 100,000 zinazoingizwa nchini kila mwaka hivyo, muafaka uliofikiwa uterejesha
biashara iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10.
Wakati
inazuia, Kenya ilisema gesi kutoka Tanzania inafungwa kiholela kwenye vituo
vilivyomo nchini humo pamoja na wafanyabiashara wake kutotoa taarifa sahihi
hivyo kutaka gesi yote kuingilia Bandari ya Mombasa ambako uratibu utafanywa.
Kenya, Tanzania zamaliza mgogoro gesi ya kupikia
Reviewed by Erasto Paul
on
July 24, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili