Wakati
wenzao wakisema makosa manne ndiyo yanayoweza kumlazimu mtuhumiwa kupimwa
mkojo, Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema inafuatilia sakata la mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi.
Lissu,
ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alikamatwa Alhamisi
akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati akisubiri
kwenda Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa jumuiya hiyo.
Wanasheria
wa Lissu wamesema waliambiwa na polisi kuwa amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi,
lakini alitakiwa kutoa kipimo cha mkojo, jambo ambalo limezua maswali.
“Tutafanya
mipango ya kufuatilia kesi ya Wakili Tundu pamoja na mchakato mwingine wowote
wa mahakama ambao umeshafikishwa mahakamani au unaweza kufikishwa mahakamani,
kwa niaba yake kuthibitisha haki za Mtanzania kama zilivyoelezwa na sheria ya
kimataifa,” inasema taarifa ya Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS)
iliyosainiwa na rais wake, Richard Mugisha.
Taarifa
hiyo pia imeeleza kuwa EALS inachukulia kukamatwa kwa Lissu kama ishara
nyingine ya kuendelea kuzorota kwa uhusiano baina ya Serikali na TLS, hali
iliyoanza wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.
“Ni kitu
kilicho wazi kuwa uhusiano huo umekuwa ukiharibika tangu kipindi cha kuelekea
na baada ya matokeo ya Mkutano Mkuu wa mwaka wa TLS ambao Wakili Lissu
alichaguliwa na wanasheria wenzake kuongoza TLS kwa mwaka mmoja,” anasema
Mugisha.
Wakati
EALS ikitoa msimamo huo, wanasheria nchini bado wanahoji sababu za Lissu
kuchukuliwa kipimo cha mkojo wakati akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi.
Kwa mujibu
wa wanasheria hao, makosa yanayoweza kusababisha mtuhumiwa achukuliwe kipimo
hicho ni ya usalama barabarani, matumizi ya dawa za kulevya, ubakaji na mashauri
ya ndoa na watoto ambayo hulazimu mkemia kupima sampuli hizo.
Hata
hivyo, katika hali iliyoibua maswali chekwa, Lissu aliyekamatwa kwa makosa ya
uchochezi, juzi alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya kupimwa
mkojo.
“Watu
wanaotumia dawa za kulevya wanalazimishwa na sheria kupimwa mkojo ili kuondoa
shaka, lakini mtuhumiwa wa uchochezi halazimishwi kupimwa mkojo,” alisema
mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse
aliyeulizwa kuhusu tuhuma zinazoweza kusababisha kuchukuliwa kwa kipimo hicho.
“Mtuhumiwa
anaweza kukataa kupimwa mkojo kwa amri. Polisi nao hawaruhusiwi kutumia nguvu.
Wanachoweza kufanya ni kutafuta amri ya mahakama ili kumlazimisha mtuhumiwa
kukubali kupima au akabiliane na kifungo kwa kukaidi amri ya mahakama.”
Maoni ya
Dk Jesse yanalingana na mwanasheria mwingine, Hudson Ndusyepo ambaye alisema
Sheria ya Vinasaba vya Binadamu ya mwaka 2009 imebainisha watu au mamlaka
zinazoweza kutaka sampuli kutoka kwa mtuhumiwa kwa masuala ya undugu, usalama barabarani
au matumizi ya mihadarati.
“Wananchi
wana haki ya kukataa vipimo ambavyo vinakinzana na sheria za nchi. Ikitokea
(polisi) wakatumia nguvu badala ya utaalamu, basi sheria itawaweka kwenye
matatizo zaidi,” alisema Ndusyapo, “Lissu alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi
ambazo hazina uhusiano wowote na kupima mkojo kama polisi walivyotaka. Kwa
hiyo, Lissu alikuwa sahihi kukataa kupima mkojo.”
Mwanasheria
mwingine, Benedict Isahabakaki alisema kitaalamu, polisi walitakiwa kumweleza
mtuhumiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili na kifungu cha sheria ambacho wanadhani
amekivunja.
“Vipimo
vya mkojo havina uhusiano wowote na makosa ya uchochezi. Tatizo ni kwamba
polisi wamekuwa wakifanya kazi zao kienyeji, ndiyo maana wanawakamata
watuhumiwa wengi Ijumaa wakidhani kwamba hawawezi kutoa dhamana siku za
wikiendi, kitu ambacho ni makosa. Polisi wanatakiwa kufanya kazi hata wikendi,”
alisema mwanasheria huyo.
Lakini
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema uchunguzi wa polisi
hauna mipaka na kwamba jeshi hilo halifanyi kazi kwa mihemko ya watu, bali kwa
kuzingatia weledi.
Alisema
kitendo cha watu kuhoji suala la Lissu kupimwa mkojo ni kuingilia uchunguzi.
Alisema uchunguzi ni suala pana, hivyo kuwataka wasubiri mtuhumiwa huyo
atakapofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yake.
“Kwenye
suala la ku-suspect (kutuhumu), polisi anaweza ku-suspect anything (kitu
chochote) kutoka kwa mtu yeyote. Siwezi kuelezea mikakati na mbinu za
kiuchunguzi, lakini mtambue kwamba uchunguzi is too general (ni mpana), unaweza
kuchunguzwa kwa mambo mengi,” alisema Mwakalukwa.
Jumuiya ya wanasheria Afrika Mashariki kufuatilia kesi za Lissu
Reviewed by Erasto Paul
on
July 24, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili