Mkuu wa
Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewataka wanaume kuacha tabia ya kuwakimbia
watoto wao, pale wanapobaini kuwa na ulemavu.
Kasesela
amesema familia nyingi zenye watoto walemavu zinalelewa na wanawake peke yao,
baada ya waume kuona hawastahili kuwalea watoto hao kutokana na unyanyapaa.
Akizungumza
jana jioni baada ya kuwatembelea watoto wenye ulemavu wanaolelewa kwenye kituo
cha Nyumba Ali cha Wilolesi, Iringa Mjini, Kasesela amesema watoto wenye
ulemavu wana haki ya kupendwa na kutunzwa na wazazi wote wawili.
“Nasikitishwa
na wanaume wanaowatelekeza watoto wao kisa ulemavu? Kwanini muwakimbie watoto
wenu kisa ulemavu? Hawa ni watoto kama walivyo wengine na wakipewa haki zao
wanaweza kufanikiwa. Msiwaachie wanawake mzigo huu wa malezi,” amesema.
Amewaagiza
maofisa tarafa kwenye wilaya hiyo kufanya utafiti nyumba hadi nyumba ili
kubaini kama kuna watoto wenye ulemavu waliofungiwa ndani ili wasaidiwe.
Mbunge wa
Viti Maalum Mkoani Iringa, Ritha Kabati amesema watoto wenye ulemavu
wanaposaidiwa kutengeneza msingi wa maisha yao, wanaandaliwa mazingira mazuri
ya kujitegemea wanapokuwa watu wazima.
“Tusipowekeza
kwa hawa watoto maana yake tunaandaa omba omba, wote tumeshuhudia baadhi ya
walemavu wakifanya vizuri lakini hadi, kuwe na mtu wa kuwashika mkono. Hili ni
jukumu letu,” amesema.
Awali,
Mratibu wa kituo hicho, Adam Duma alisema walikianzisha kwa lengo la
kuwakusanya na kuwasaidia watoto wenye ulemavu waliokuwa wamefungiwa nyumbani
kwa kukosa msaada.
Amesema
pia kituo hicho kililenga kuwakusanya wazazi na kuwaelekeza namna ya kuwalea
watoto wao wenye ulemavu ili hatimaye wafikie ndoto zao za kimaisha, ikiwamo
kupata elimu.
“Tumefanikiwa
kuwakutanisha wazazi ambao wameweza kuwa na sauti moja katika kubainisha na
kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii ya watoto
waishio na ulemavu,” alisema kiongozi huyo.
Amesema
kuwa wamefanikiwa kuwa na vituo viwili vya watoto wenye ulemavu na kwamba
kila kituo kina watoto 35.
“Majukumu
yetu mengine ni kuwafanyia watoto hao mazoezi ya viungo kwa sababu wapo wanaopata
ahueni na wengine kurejea kwenye hali ya kawaida, kutokana na mazoezi hayo,”
amesema.
“Kituo
hiki kwa msaada wa wahisani mbalimbali na mahitaji makubwa ni chakula, baiskeli
za walemavu pamoja na gharama za uendeshaji,” ameongeza.
Kasesela awasuta wanaume wanaowakimbia watoto walemavu
Reviewed by Erasto Paul
on
July 18, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili