Wakili wa
kujitegemea, Alex Balomi ameifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kuwa Harbinder Singh Sethi anaumwa, hali yake imeendelea
kubadilika na hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi.
Balomi
aliyaeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi mara baada ya
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,
Leonard Swai kuieleza mahakama kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na
upelelezi wake bado haujakamilika.
Baada ya
kutolewa maelezo hayo na Swai, Wakili Balomi ameiambia mahakama hiyo kuwa
Sethi anasumbuliwa na uvimbe tumboni ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa
madaktari.
“Kutokana
na hali yake kuwa mbaya hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi hivyo
anahitaji ungalizi wa karibu wa madaktari na kwamba
wamebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari,” Balomi
aliifahamisha mahakama.
Balomi
aliongeza kuwa hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika
Kusini.
Swai
amesema nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka kuziwasilisha
mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya
kisheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika mahakamani
kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.
Kutokana
na hoja hizo, Hakimu Shaidi amesema suala la ugonjwa si la kufumbiwa macho,
linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuelekeza magereza kufanya kila
linalowezekana kuhakikisha hali ya mshtakiwa huyo inabaki katika hali
nzuri na inapobidi wawasiliane na wataalam wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili.
Kesi
imeahirishwa hadi Julai 28, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama
upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Katika
kesi hiyo, Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu
uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa
nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha
fedha na kusababisha hasara ya Dola 22, 198,544.60 sawa na Sh
309,461,300,158.27.
Hali ya Sethi yabadilika, augua tumbo
Reviewed by Erasto Paul
on
July 14, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili