Dude linalowatesa vigogo magerezani





Katika siku za karibuni watu maarufu katika maeneo tofauti-kuanzia serikalini, michezoni, wanasheria hadi wafanyabiashara wakubwa- wamejikuta mikononi mwa vyombo vya dola, wengi wakikabiliwa na mashtaka mawili makubwa; utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.
Baadhi wamekaa mahabusu kwa muda mrefu na wengine ndio kwanza wameingia na wengine wameshakiri kosa na hukumu kutolewa.
Wote wanalazimika kwenda mahakamani kuhudhuria hatua za mwanzo wakitokea mahabusu kwa kuwa utakatishaji fedha hauna dhamana na uhujumu una sharti gumu la dhamana.
Zaidi ya watu tisa maarufu wameshashtakiwa kwa makosa hayona dalili zinaonekana kuwa idadi inaweza kuongezeka.
Siku za nyuma vigogo kama hao waliishia kushtakiwa kwa makosa ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yaliyowawezesha kwenda mahakamani wakitokea majumbani baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Ukizingatia uwezo mkubwa wa kifedha waliokuwa nao, wengi wa watu hao, ama hawakuonja kabisa rumande au walikaa kwa siku chache na kuachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Lakini hali imebadilika.
Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya yuko mahabusu akikabiliwa na makosa tofauti, mojawapo likiwa la utakatishaji fedha; wakili maarufu wa Arusha, Median Mwale pia yuko ndani kwa zaidi ya miaka mitano pia akiwa na shtaka kama hilo.
Si hao tu, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji pia amesomewa mashtaka kama hayo, hali kadhalika Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wafanyabiashara maarufu, James Rugemalira na Harbinder Sing Seth.
Hao ni baadhi ya watu maarufu walio mahabusu hadi sasa kwa makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.
“Ni utekelezaji tu wa sheria. Sheria ilikuwepo na pengine utekelezaji ulikuwa dhaifu ndio maana sasa mnaona matukio mengi,” alisema mwanasheria wa jijini Dar es Salaam, Ramadhan Maleta alipoulizwa sababu za kuongezeka kwa kesi zinazohusu utakatishaji fedha.
“Watu walikuwa wakitakatisha fedha tangu zamani na sheria ilikuwepo na mahakama ni zilezile. Kwa hiyo nadhani ni utekelezaji tu.”
Sheria ya utakatishaji fedha ilitungwa mwaka 2006 na FIU ilianza kufanya kazi mwaka 2007, wakati dunia ikipambana na jinai hiyo inayohusishwa kwa kiasi kikubwa na biashara ya dawa za kulevya na ugaidi.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2014/15 ya Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU), utakatishaji fedha ni neno linalotumiwa kuelezea “kitendo cha kuficha chanzo cha fedha haramu na kuzihamishia kisiri katika biashara halali kwa lengo la kuzilinda zisifuatiliwe au kutaifishwa na Serikali”.
Takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Fedha Haramu (UNODC), kiwango cha fedha kinachotakatishwa kwa mwaka ni kati ya asilimia 2-5 ya pato la dunia, ingawa timu iliyoundwa na nchi tajiri duniani kufanya utafiti wa tatizo hilo, FATF ilisema si rahisi kujua kiwango hicho kutokana na asili ya vyanzo hivyo.
Kwa mujibu wa taasisi ya PWC, kiwango cha fedha za kupambana na tatizo la utakatishaji fedha kinaweza kukua hadi kufikia dola 8 milioni za Kimarekani mwaka huu.
Wimbi la vigogo kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kuhujumu uchumi linalounganishwa na utakatishaji fedha, limeongezeka katika siku za karibuni.
Kitilya, ambaye alishastaafu, ameshtakiwa pamoja na aliyewahi kuwa mkuu wa uwekezaji wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon.
Pamoja na mashtaka mengine, watatu hao wanadaiwa kutakatisha dola5 milioni za Marekani kwa kuzihamisha kutoka katika akaunti ya kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Ltd (EGMA).
Wanahusishwa na dola 6 milioni zilizokwenda kwa kampuni ya usimamizi wa uwekezaji wa mitaji, EGMA kutokana na mkopo wa dola 600 milioni ambao Serikali ilipata kutoka benki za nje.
Aliyekaa mahabusu kwa muda mrefu ni Mediam Mwale ambaye anadaiwa kukutwa na fedha haramu zaidi ya Sh18 bilioni.
Mwale, ambaye Agosti 2, 2011 alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Charles Magesa alikataa kupokea hati ya mashtaka baada ya kugundua makosa ya kisheria.
Vigogo wengine waliokumbwa na tuhumu hizo ni Rugemalira, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki sehemu ya IPTL na Harbinder Sethi ambaye ni mmiliki wa sasa. Wanahusishwa na fedha zilizochotwa Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na IPTL na Tanesco zilizokuwa katika mgogoro wa kimkataba.
Utekelezaji wa sheria hiyo haukuiacha taasisi ya michezo salama. Malinzi, (rais wa TFF), Celestine Mwesiga (katibu wa TFF), Nsiande Mwanga (mhasibu TFF), Evans Aveva (rais wa Simba) na Geofrey Nyange (makamu wa rais Simba) wako mahabusu kwa tuhumu za kutakatisha fedha.
Malinzi na Mwesiga wanahusishwa na miamala kadhaa ya jumla ya dola514,618 za Marekani (Shilingi 1.1 bilioni) kutoka akaunti za TFF kwenda akaunti binafsi, kama ilivyo kwa Aveva na Nyange, ambao wanahusishwa na fedha kutoka akaunti ya klabu hiyo kubwa kwenda akaunti binafsi.
Muathirika mpya ni Manji ambaye juzi alisomewa mashtakiwa saba ya uhujumu uchumi akiwa kitandani Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Anadaiwa kukutwa na vitambaa vyenye thamani ya Sh44 milioni ambavyo ni mahususi kwa ajili ya kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Ingawa kosa lake linadhaminika, uwezekano wa kupata dhamana  utategemea kutoongezewa shtaka la utakatishaji fedha.
Jana mkurugenzi wa kampuni ya Golden Shark Mining Ltd, Cuthbert Kshululi, 48, alifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alikosomewa mashtaka tofauti, likiwamo la kutakatisha dola2,405, 000 za Kimarekani (Sh5.3 bilioni).
Anadaiwa kupata fedha hizo kutoka kwa Holism Group Ltd kwa ahadi ya kujipatia kilogramu 500 za madini ya  dhahabu kupitia kampuni yake ya Golden Shark Mining Ltd wakati akijua ni uongo.
Lakini wakili wa siku nyingi nchini, Martin Matunda anasema pamoja na sheria ya utakatishaji fedha kuwa nzuri, inaweza kutumika vibaya.
“Utakatishaji fedha ni kuficha chanzo cha fedha haramu kwa lengo la kuzipeleka kwenya uwekezaji au shughuli yoyote halali. Sasa hivi naona hatari ya watu wanaofanya wizi wa kawaida tu kubandikwa shitaka la utakatishaji fedha haramu,” alisema Matunda.
Sheria ya Uhujumu Uchumi
Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi ilianzishwa mwaka 1984 na imefanyiwa marekebisho kadhaa. Kwa mujibu wa kifungu cha 36 (1) Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi, mahakama inaweza kumpa dhamana mtu yeyote aliyeshtakiwa chini ya sheria hiyo endapo ataomba dhamana.
Sharti pekee gumu katika sheria hiyo ni kifungu kidogo cha 5 (a) kinachoitaka mahakama kutoa sharti la mshtakiwa kuweka mahakamani dhamana ya nusu ya thamani ya fedha anazodaiwa kuhujumu.
Sheria ya utakatishaji fedha
Tanzania ilipitisha rasmi mwaka 2006 sheria inayoweka vifungu vinavyoharamisha utakatishaji fedha ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kimataifa kuzuia fedha zinazotokana na biashara haramu kama ya dawa ya kulevya na kutumika kufadhili ugaidi.
Kwa mujibu wa sheria hii, mabenki na taasisi za kifedha, wauzaji wa fedha, wahasibu, mawakala wa kuuza ardhi, wauza madini, maofisa forodha, mawakili, maofisa wanaosaidi wateja katika kuandaa au kutekeleza miamala, wana jukumu la kisheria la kutoa taarifa kuhusu miamala yote watakayoitilia shaka au kuona dalili za utakatishaji fedha.
Makundi mengine ambayo sheria hiyo inawatambua kama watoa taarifa ni mawakili au maofisa wanaoshughulika na mashirika ya biashara, usimamizi wa fedha, dhamana, ufunguzi au usimamizi wa akaunti za benki, akaunti za akiba au orodha ya fedha zilizowekwa kwa faida, na ununuzi au uuzaji wa taasisi za kibiashara na mengineyo.
Pia kifungu cha 4 (1) cha sheria hiyo kimeanzisha Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu (FIU).
Makosa ya kutakatisha fedha
Kwa mujibu wa sheria hiyo, makosa ya utakatishaji fedha haramu ni pamoja na wizi, magendo, kujipatia fedha au mali kwa vitisho, kugushi nyaraka, ukwepaji wa kodi, uvuvi haramu, uchimbaji haramu wa madini na uhalifu wa mazingira.
SOURCE-MWANANCHI

Dude linalowatesa vigogo magerezani Dude linalowatesa vigogo magerezani Reviewed by Erasto Paul on July 07, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.