Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara,
Chelestino Mofuga, amepiga marufuku uchimbaji wa madini ya dhahabu kwenye
machimbo ya Haydom hadi hapo mwekezaji atakapokamilisha mkataba na Halmashauri
ya wilaya hiyo.
Pia, Mofuga
ameagiza kukamatwa kwa mmiliki na dereva wa lori la tani 10 lililokutwa
limebeba mchanga wa dhahabu (makinikia) kutoka machimbo ya Haydom likipeleka
mkoani Singida kuchenjua.
Akizungumza
jana (Alhamisi Julai 6) kwenye machimbo hayo amesema aliamua kufanya ukaguzi wa
kushtukiza kwenye machimbo ya dhahabu ya Haydom na kukuta lori la tani 10
likiwa na mchanga unaopelekwa mkoani Singida.
Amesema alipata
taarifa kuwa lori hilo lilishabeba mchanga huo zaidi ya mara sita kabla ya
kukamatwa na kuamuru kusitisha kwa zoezi hilo la kwenda kuchenjua dhahabu hiyo
mkoani Singida badala ya Haydom.
“Nimeagiza
mmiliki na dereva wa lori hilo lenye namba za usajili T662 AWT, mali ya Mohamad
Ally mkazi wa jijini Arusha kushikiliwa kwenye kituo cha polisi Haydom hadi
uchunguzi ufanyike,” amesema Mofuga.
Amesema ametoa
amri ya kusitishwa kwa uchimbaji wa dhahabu kwenye eneo hilo hadi mwekezaji
atakapokamilisha mikataba na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Hudson
Kamoga.
Baaadhi ya
wananchi wa eneo hilo, walipongeza hatua ya mkuu huyo wa wilaya kuchukua hatua
hiyo kwani baadhi ya watu wanaojiita wawekezaji wamekuwa wanapora hovyo hovyo
rasilimali za nchi.
Mkazi wa
Haydom, Raymond Sulle amesema walishangazwa na kitendo cha mwekezaji huyo
aliyekuwa anabeba mchanga huo wa dhahabu na kuondoka nao hadi Singida kuchenjua
badala ya Haydom.
“Baada ya tukio
hio tulitoa taarifa mara moja kwa mkuu wetu wa wilaya, ambaye naye hakuchukua
muda mrefu akafika kwenye eneo hilo na kuagiza zoezi hilo lisimame mara moja,”
amesema Sulle.
DC Mbulu apiga marufuku uchimbaji dhahabu
Reviewed by Erasto Paul
on
July 07, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili