Waziri wa
Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amemtunuku Dk Jane Goodall tuzo
maalumu ya kutambua mchango wake katika kuwatunza sokwe kwenye Hifadhi ya Taifa
ya Gombe.
Mbali na
tuzo hiyo, Profesa Maghembe, kwa niaba ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa),
amemkabidhi Dk Goodall zawadi mbalimbali ikiwamo cheti cha kutambua mchango
wake, sanamu ya sokwe pamoja na picha ya sokwe.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Profesa Maghembe
amesema Dk Goodall ametoa mchango mkubwa kwenye sekta ya uhifadhi kwa
kubainisha tabia za sokwe ambazo watu wengi hawazijui.
Amesema
mwanamke huyo ambaye ni raia wa Uingereza amebainisha katika tafiti zake kwamba
sokwe wanafikiri na wana hisia kama walivyo binadamu.
Waziri
Maghembe ameitaka taasisi ya Jane Goodall ambayo inafanya tafiti mbalimbali za
wanyama kufundisha Watanzania hapa nchini ili waendeleze kazi kubwa aliyokuwa
akiifanya.
"Dk
Goodall amejenga timu ya watafiti na anatambulika duniani kote. Serikali pia
tunatambua mchango wake katika uhifadhi wa sokwe, kazi ambayo ameifanya kwa
muda mrefu," amesema Profesa Maghembe.
Kwa upande
wake, Dk Goodall amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Tanapa kutambua mchango
wake katika utunzaji wa sokwe, jambo ambalo anasema limempa nguvu ya kuendelea
na kazi hiyo.
Dk Goodall
amesema alizaliwa akiwa anapenda sana wanyama na alikuwa na ndoto ya kuja
Afrika kuangalia wanyama, ndoto ambayo aliitimiza mwaka 1960.
"Nikiwa
msichana mdogo, wenzangu walinicheka nilipowaambia nataka kwenda Afrika. Lakini
nilipokuja na kwenda kuwasimulia kuhusu sokwe walifurahi na kuja kutembelea
hifadhi mbalimbali za Tanzania," amesema Dk Goodall.
Apewa tuzo kwa kutunza sokwe vizuri
Reviewed by Erasto Paul
on
July 14, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili