Dodoma. Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kuokoa Sh53.9 bilioni
kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizofanywa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika mwaka 2016/2017.
Amesema kiasi
hicho cha fedha ni kikubwa mno ikilinganishwa ni Sh7.0 bilioni ambazo
zilizookolewa katika mwaka 2015/2016 na taasisi hiyo.
Majaliwa ametoa
kauli hiyo leo Ijumaa, wakati akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge wa
Afrika walio katika Mapambano ya Rushwa (APNAC) tawi la Tanzania kwenye ukumbi
wa African Dream mjini Dodoma.
Akizungumzia
hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa,
Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi wa
umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea kupungua.
“Baadhi ya
hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya Takukuru,
kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya
kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu katika
utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za kisheria dhidi
ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” amesema.
Amewaomba
wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali kwani haina mzaha kwenye mapambano
hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa na tutaendelea na
mapambano hayo. Hivyo, ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono
katika mapambano haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono
kwenye vita hii,” amesisitiza.
“Tayari
tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi, uchukuzi,
biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea kuiwezesha Takukuru
ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza ya kubaini mianya na kutoa ushauri wa
kuziba mianya hiyo ya rushwa. Lengo letu ni kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa
kuwa kinga ni bora kuliko tiba”.
Takukuru yaisaidia Serikali kuokoa Sh53 bilioni
Reviewed by Erasto Paul
on
June 09, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili