Dar es Salaam. Viongozi wa mashirika ya Umma na Binafsi wametakiwa
kujenga mazoea ya kupima afya zao mara kwa mara ili endapo watabainika kuwa na
magonjwa, wapate matibabu mapema.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed
Janabi wakati akiongea na viongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
waliofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya upimaji wa afya zao.
Profesa Janabi amesema baadhi ya
viongozi hawana mazoea ya kupima afya zao japo mara moja kwa mwaka na inapotokea
wamegundulika kuwa na tatizo la ugonjwa huwa ni kubwa na
limeshaleta madhara mwilini.
“Wanapokuja kugundua tatizo,
wakati mwingine huwa ni vigumu kutibika, lakini tatizo kama
hilo likigundulika mapema katika hatua ya awali huwa ni
rahisi kutibika,” amesema.
Akizungumzia kuhusu magonjwa ya moyo
Profesa Janabi amesema ni muhimu mgonjwa afuate maelekezo ya jinsi ya kutumia
dawa aliyopewa na daktari wake kwani kuna baadhi ya wagonjwa wamekuwa na tabia
ya kuacha kutumia dawa pindi wanapojiona wamepata naafuu jambo ambalo siyo
sahihi.
Akielezea jinsi ya kujikinga na
magonjwa ya moyo kwa upande wa chakula Ofisa Lishe kutoka JKCI, Louisa Shem
amesema ni muhimu kupunguza utumiaji wa vyakula vya mafuta kupita kiasi hasa
mafuta yatokanayo na wanyama na kutumia vyakula vya nafaka zisizokobolewa.
“Kupunguza unywaji wa pombe na
uvutaji wa bidhaa zitokanazo na tumbaku ikiwamo sigara, kufanya mazoezi ya
mwili angalau nusu saa kwa siku na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye chumvi
nyingi,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Afya
na Usalama Kazini kutoka Shirika la Nyumba la NHC, Dk Yothan Mackenzie
amesema hivi karibuni walikuwa na mkutano wa baraza la wafanyakazi katika
mkutano huo kulikuwa na mada ya ulaji na afya wakaona ni vyema mada hiyo iende
sambamba na upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwamo ugonjwa wa moyo.
Dk Mackenzie amesema wanawapima
viongozi hao kwa awamu hadi sasa jumla ya wakurugenzi na wakuu wa vitengo 14
wamepima na kujua afya zao na viongozi wengine wataendelea kupima kwani shirika
lao linaamini kuwa mfanyakazi akiwa na afya njema ataweza kufanya kazi zake
vizuri.
Baadhi ya magonjwa waliyopima
viongozi hao ni pamoja na moyo, tezi dume, figo na sukari.
Viongozi wa mashirika ya umma, binafsi watakiwa kupima afya
Reviewed by Erasto Paul
on
June 09, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili