Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya.
MAMBO yanazidi kuwa magumu kwa
wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu baada ya asilimia ya marejesho ya
mkopo huo kwa kila mwezi kuongezeka kutoka 8% hadi 15%.
Mabadiliko haya yamekuja baada ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuwa tayari
amekwishasaini mabadiliko ya sheria yanayomtaka mwajiri kukata asilimia
15 ya mshahara wa mwajiriwa ambaye ni mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu
kwa ajili ya kulipa deni lake analodaiwa na Bodi ya Mikopo.
Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul Razaq, wakati akitangaza kutoa siku 3
kwa wadaiwa sugu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi wa Urejeshaji wa Mikopo, Abdul Ally.
Hatua hii imekuja ikiwa
wadaiwa hao tayari wamepewa siku 30 na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul Razaq, aliyesema wadaiwa hao
sugu watachukuliwa hatua kali iwapo hawatarejesha mikopo hiyo ndani ya
mwezi mmoja.
Katika maelezo yaliyotolewa jana na
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella
Manyanya, wakati akijibu maswali ya wananchi kupitia kipindi cha
KIKAANGONI kinachoendeshwa kupitia mtandao wa facebook wa East Africa
Television, Naibu Waziri Manyanya alisema sheria hiyo tayari imesainiwa
na siku za hivi karibuni itaanza kutumika.
“Hii asilimia 15, kimsingi ninavyofahamu
ilishasainiwa, baada ya hapo kuna kuiangalia iendane na kanuni zetu,
baada ya kuicheki imeendana na kanuni zetu kama kuna sehemu itahitaji
kuboreshwa kidogo haitazidi miezi miwili au mitatu, baada ya hapo
tutaweza kutumia hiyo 15%, na asilimia 15 ya safari hii ni tofauti na
siku za nyuma, siku za nyuma tulikuwa tunachaji asilimia 8”, alisema
Manyanya.
Hapo awali wadaiwa hao wa mikopo
walikuwa wanakatwa asilimia 8, lakini sheria ya sasa itaruhusu wadaiwa
wa mikopo ya elimu ya juu kukatwa asilimia 15 ya kipato chao.
Pia Manyanya amesisitiza kuwa kwa
wale ambao hawajaajiriwa, lakini wanafanya biashara zao wanatakiwa
kuwasilisha angalau shilingi 120,000 kila mwezi na kuwashauri kuwa ni
vema wakapeleka zaidi ili wamalize haraka madeni yao.
Kuhusu wasio na kazi,
amesema haiwezekani mtu asome halafu akose shughuli ya kufanya na
kuwataka kutafuta shughuli yoyote ya kufanya ili waanze mapema kulipa
madeni yao ndani ya miaka miwili baada ya kuhitimu masomo.
Mambo Yazidi Kuwa Magumu kwa Wadaiwa Bodi ya Mikopo, Sasa Kukatwa 15% ya Kipato Chao kwa Mwezi
Reviewed by Erasto Paul
on
December 01, 2016
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili