Wanawake wanaendesha malori, mabasi, treni na ndege, ni makondakta wa daladala na shughuli nyingine ambazo awali zilidhaniwa kuwa zinawafaa wanaume pekee.
Kazi pekee
inayoonekana pengine kuwa rahisi, kuendesha gari ndogo za abiria, yaani teksi
kwa kuwa ni kawaida kuwaona wanawake, hata wasichana wadogo wakiendesha vyombo
hivyo.
Hiyo
ilikuwa nadra sana kwa mwanamke kuendesha teksi ambazo hufanya kazi hadi usiku
mwingi.
Lakini,
jijini Dar es Salaam mwiko huo umeshakoma; wanawake sasa ni madereva wa magari
hayo madogo ya abiria, lakini wakiwa wamewezeshwa na kampuni ya Uber
iliyorahisisha huduma ya usafiri kwa kutumia teknolojia ya simu.
Na
wanawake hao ni mchanganyiko; kuanzia wasomi hadi wenye elimu ya kawaida.
“Wakati
nikiwa Nairobi, nilitumia app ya Uber. Niliipakua kwenye simu yangu na mtu
ambaye alikuja kunichukua (kwa gari) alikuwa mwanamke,” alisema Suma Mwaitenda
(34), mthamini na mhadhiri wa Chuo Kikuu Ardhi ambaye sasa ni dereva wa Uber.
“Nilivutiwa
na ujasiri wake. Mwanamke yule alinieleza uzoefu wake na aliingiaje katika
shughuli ya Uber. Alisema waliwahi kuajiriwa lakini akaacha kazi baada ya kuona
fursa ya Uber.”
Suma,
ambaye alikuwa akizungumza na Esther Kibakaya wa gazeti la The Citizen, alisema
alihamasika na kuamua kwamba akirejea Tanzania angewashirikisha wenzake, hasa
wanawake kuhusu fursa hiyo.
“Nilijiambia
kuwa kama nataka watu waamini kuwa inawezekana, lazima niwe wa kwanza kufanya
hilo,” alisema Suma, ambaye ni ofisa mtendaji wa taasisi ya Uhuru Women Club.
Suma
anamudu kufanya kazi hiyo pamoja na ya uhadhiri na kulea familia yake.
“Kwa
kawaida ninatenga saa tatu hadi nne kwa siku kulingana na ratiba yangu ya
kufundisha. Wakati mwingine naweza kuwa ninatakiwa kufundisha chuoni asubuhi
hadi mchana kwa hiyo napata muda saa 10:00 jioni,” alisema.
“Kama
ikitokea nina miadi mjini, basi nawasha app ya Uber ili nichukue abiria kama
inavyokuwa naporejea. Kwa kifupi nafanya kazi hii kadri navyopata muda,”
alisema Suma.
Suma
hakuanza kazi hiyo kinyemela; alimshirikisha mumewe na ilichukua muda mrefu
kumshawishi hadi kukubali.
Anasema
kazi hiyo ina changamoto zake kama zilivyo nyingine, kubwa ikiwamo ya
kutongozwa na abiria, lakini anasema anaweza kukabiliana nazo.
Suma
anashauri wanawake wenzake waone fursa ya kutumia magari yao kibiashara badala
ya kuyaacha yakae bila ya shughuli zozote.
Suma si
mwanamke pekee aliyeingia kwenye biashara hiyo.
Happiness
Mremi, mhitimu wa shahada ya elimu katika Chuo Kuu cha St Augustine, Angelina
Shonza, aliyehitimu shahada ya ustawi wa jamii, Pascalia Dominic na Prisca
Kabendera ni baadhi tu ya wanawake wanaofanya kazi hiyo.
Baada ya
kumaliza masomo yake mwaka 2015, Happiness alianza kujishughulisha na kilimo
cha mpunga mkoani Mwanza na baadaye biashara ya nguo eneo la Kariakoo, lakini
mambo hayakwenda vizuri.
“Ilikuwa
ni wakati huo nilipomsikia mmoja wa marafiki wa familia aliyetutembelea
akizungumzia Uber,” alisema Happiness.
“Nilimwambia
mume wangu na akanieleza jinsi biashara ilivyo. Nilipomwambia kuwa nataka
nifanye, alinijibu kuwa siwezi kufanya kitu kama hicho,” alisema Happiness.
“Nilifanya
uchunguzi na kufurahia zaidi wazo hilo na kumwambia mume wangu kuwa nataka kuwa
dereva wa Uber kwa sababu gari langu linaegeshwa tu nyumbani bila ya kazi.
Alikataa kabisa, ikafika wakati ikawa kila nikitaja Uber kunazuka majibizano
makali.”
Baadaye
alifanikiwa kumshawishi baada ya kwanza kutembelea ofisi za Uber na kuonyeshwa
jinsi mfumo huo unavyofanya kazi.
Naye
Shonza anasema wazo la kukaa bila ya kazi wakati kulikuwa na kitu ambacho
angeweza kufanya kupata fedha, ndilo lililomsukuma kuwa dereva wa Uber.
“Mtu wa
kwanza kumwambia alikuwa mume wangu, lakini aliniambia si kazi nzuri kwa
mwanamke kwa sababu ni kazi ngumu kushinda usiku mzima umekaa ukiendesha gari.
“Hata
hivyo, hilo halikunizuia kujaribu. Nilijaribu na baadaye kuanza kazi kama
dereva kamili, nikifanya kazi kuanzia saa 10:00 au saa 11:00 alfajiri hadi saa
2:00 usiku,” alisema Shonza.
Shonza
ameshafanya kazi hiyo kwa miezi mitano sasa na hajutii uamuzi wake, akiwa anajipatia
Sh2 milioni hadi 2.5 milioni kwa mwezi.
Wanawake wasomi madereva wa teksi Dar
Reviewed by Erasto Paul
on
October 01, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili