Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameagiza maofisa waliohusika na miradi 33
katika taasisi 17 ambazo ununuzi umebainika kuwa na viashiria vya rushwa
kupelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru).
Dk Mpango
ametoa agizo hilo leo Ijumaa mjini hapa baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya
utendaji wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA)
kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Amesema taarifa
hiyo ni muhimu kwa sababu fedha za umma zaidi ya asilimia 70 zinatumika kwa
ajili ya kununua vifaa na huduma zinazotumiwa na taasisi za Serikali, hivyo
watafanya utaratibu wa uwajibikaji kisheria kuwasilisha ripoti hiyo bungeni na
atafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.
Akizungumza
kabla ya kukabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Dk Matern Lumbanga
amesema taasisi 81 kati ya 112 zilifanyiwa ukaguzi wa kupima thamani halisi ya
fedha.
Pia,
mikataba ya miradi 345 ilikaguliwa na kati ya hiyo 87 ilipata alama za kiwango
cha kati na saba ilipata alama za kiwango kisichoridhisha.
Amesema
katika ukaguzi huo, walibaini malipo yenye utata katika taasisi
tatu ya
Sh483.44 milioni zilizolipwa kwa makandarasi lakini hakuna kazi ambazo zilikuwa
zimefanyika.
Dk
Lumbanga amezitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Amesema
katika tathmini iliyofanywa na PPRA miradi 33 katika taasisi 17 ilibainika kuwa
na kiwango kikubwa cha viashiria vya rushwa ikimaanisha kuwepo kwa uwezekano
mkubwa wa uwepo wa vitendo vya rushwa katika taasisi hizo na miradi hiyo.
Alizitaja
kuwa ni mamlaka za maji safi na maji taka Moshi (Muwasa), Mwanza
(Mwauwasa), Arusha (Auwasa), halmashauri za wilaya za Msalala,
Kibondo na
Moshi.
Nyingine
ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela; Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Chuo cha Ufundi Arusha,
Halmashauri
ya Mji wa Kahama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Uhasibu ya Arusha
(IAA), Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Mji wa Masasi na Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha
Arusha
(AICC).
Kuhusu
uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa sheria na kanuni, Dk Lumbanga amesema mwaka
jana wa fedha walifanya uchunguzi wa tuhuma nane zilizohusu mikataba 10 ya
ununuzi iliyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh280 bilioni.
“Uchunguzi
huu ulitokana na maagizo kutoka mamlaka za juu au maombi
kutoka
taasisi zenyewe,” amesema.
Amezitaja
taasisi hizo kuwa ni TRA, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI),
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Shirika la Bima la Taifa (NIC),
Mamlaka ya
Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga
(TCAA),
Wizara ya Fedha na Mipango na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema
uchunguzi huo ulibaini taasisi sita za TRA, MOI, Nida, NIC, TCRA na Halmashauri
ya Wilaya ya Kondoa ziliisababishia Serikali hasara ya Sh12.2 milioni kutokana
na sababu mbalimbali.
Sababu
hizo amezitaja kuwa ni ucheleweshwaji wa malipo kwa makandarasi uliosababisha
ongezeko la riba na faini zilizotokana na ukiukwaji wa
utaratibu
wa kijamii na mazingira kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa kazi za ujenzi.
“Kutokana
na uchunguzi huo, PPRA iliweza kuingilia kati mchakato wa zabuni tatu zenye
thamani ya Sh42.97 bilioni baada ya kujiridhisha kuwa Serikali isingepata
thamani halisi ya fedha,” amesema.
Mwenyekiti
huyo amesema uchunguzi huo ulibainisha kuwa Serikali ingeokoa takriban Sh1.61
bilioni kama taasisi husika zingetekeleza maelekezo ya mamlaka hiyo.
UKAGUZI PPRA WAIBUA MAZITO 0
Reviewed by Erasto Paul
on
September 29, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili