Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90 kuanzia leo.
Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan
Abbasi amesema leo Alhamisi kuwa agizo hilo pia linahusu toleo la
mtandaoni.
Dk
Abbasi amesema adhabu hiyo inatokana na toleo namba 529 la Septemba 27
hadi Oktoba 3 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “Urais
utamshinda John Magufuli.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amesema wameambiwa sababu ya kusitishwa kwa gazeti hilo ni habari hiyo.
Ulimwengu amesema kwa sasa wanashauriana kuona ni nini cha kufanya.
Dk
Abbasi amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali
inasisitiza uchambuzi huo ni maoni ya Raia Mwema ya haki (fair
comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo
ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John
Magufuli.
Amesema gazeti hilo pia limewahi kuonywa kwa makosa mbalimbali.
Amesema
nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata kusema
ni, “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na “Watakaobaki
Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”
Dk
Abbasi amesema walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya nchi
Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa Raia Mwema waliomba muda
ambao walipewa. “Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo,
wakakiri kosa na kuomba radhi.”
Mkurugenzi
huyo amesema bado Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia mzaha
upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Tehama amani na
utulivu uliopo kwa miaka mingi utapotea na kukaribisha maafa kama
ilivyotokea kwingineko duniani.
“Serikali,
katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri
wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12,
2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa
gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa,” amesema.
Dk
Abbasi amesema kupitia hilo, wamejifunza mambo kadhaa kuhusu changamoto
za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi cha kuwalazimu
kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba
uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa
na si kufanyiwa dhihaka.
Serikali yalifungia gazeti la Raia Mwema
Reviewed by Erasto Paul
on
September 29, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili