Walioghushi vyeti kuchukuliwa hatua za kinidhamu.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema watumishi wa umma walioghushi vyeti watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kairuki amesema hayo leo (Julai 11) katika kikao kazi na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Tarafa ya Mbagala.
Amesema wote walioghushi vyeti hawapo kazini na wameshafutwa katika orodha ya malipo ya Serikali.
Waziri ameelekeza waajiri kuwafuta wote wasiostahili kuwepo katika orodha ya malipo na wasimsubiri hadi afike katika maeneo yao ya kazi ili kutekeleza agizo hilo.
“Baada ya uhakiki kukamilika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa walioghushi vyeti kwa kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyopo katika utumishi wa umma,” amesema Kairuki kama alivyokaririwa katika taarifa iliyotolewa na wizara.
Amewataka waajiri kuhakikisha wanahakiki taarifa za watumishi wapya wanapoajiriwa na wale wanaohamia ili kujiridhisha kama wana vyeti safi.
“Ni wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha kuwa vyeti vya kila mwajiriwa mpya vinathibitishwa na mamlaka husika kabla ya kumwajiri na hatimaye kumuingiza kwenye orodha za malipo ya mshahara kupitia mfumo wa HCMIS na mifumo mingine ya mishahara ya kitaasisi,” amesema.
Akizungumzia watumishi wa umma walioajiriwa na sifa za darasa la saba, Kairuki amesema endapo aliajiriwa kabla ya Mei 20 mwaka 2004 anastahili kuendelea kuwa katika utumishi wa umma na endapo kajiendeleza abadilishiwe muundo kuendana na sifa za elimu aliyopata.
Amesema endapo mtumishi huyo aliajiriwa baada ya Mei 20 mwaka 2004 anatakiwa kuwa na sifa ya elimu ya kidato cha nne.
Kairuki pia ametoa ufafanuzi wa kazi inayoendelea inayohusu kuoanisha taarifa za watumishi na zile za usajili uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
“Uhakiki huu utaongeza usahihi wa taarifa za watumishi nchini, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa zinazomhusu mtumishi na kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya kimkakati ya Tehama ili ibadilishane taarifa,” amesema.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar e Salaam, Theresia Mbando amempongeza Waziri Kairuki kwa kuboresha utumishi wa umma.
Mbando amesema sasa watumishi wa umma waliobaki kazini wameweza kuziba pengo la waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na kuondolewa kazini.
Walioghushi vyeti kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Walioghushi vyeti kuchukuliwa hatua za kinidhamu. Reviewed by Erasto Paul on July 11, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.