STORI: SIFAEL PAUL | IJUMAA WIKIENDA
MWANAMAMA Rose Muhando ni staa mkubwa wa Nyimbo za Injili Bongo. Rose ana sauti kali, lakini ya kuvutia watu, yenye kupenya vilivyo kwenye ngoma za masikio ya msikilizaji na kuibua hisia na msisimko wa aina yake.
Rose ambaye amezaliwa mwaka 1976 huko Kilosa mkoani Morogoro anajulikana kwa utunzi wa mashairi ya kumtukuza Mungu. Midundo ya nyimbo zake ni za kuchezeka kwenye ‘Disko la Yesu’.
Mbali na sifa hizo, pia ana uwezo mkubwa wa kumiliki jukwaa. Kubwa kuliko ni kwamba ana nyimbo nyingi zinazoimbika kwa watu wa rika mbalimbali bila kujali imani za kidini. Baadhi ya nyimbo zake ni Nibebe, Utamu wa Yesu, Jipange Sawasawa, Chineke, Sitanyamaza, Nipe Uvumilivu, Facebook na nyingine kibao.
KWA NINI ROSE?
Kinachonifanya kuandika makala haya ni mahojiano ya Gazeti la Ijumaa Wikienda na Rose wiki iliyopita ambayo yalijaa maswali mengi hasa nikitaka kujua ni kwa nini Rose amekuwa katika hali aliyokuwa nayo yenye kusikitisha mno?
Rose mwenye umri wa miaka 41 alilieleza Wikienda namna anavyotishiwa kuuawa na mtu aliyekuwa akimlazimisha kufanya mambo asiyoyataka na kwamba hali ni mbaya, akitamani kuhama nchi ili kuinusuru roho yake.
NI KWELI ROSE NI TEJA?
Lengo la mahojiano hayo lilikuwa ni kupata ukweli kuhusiana na skendo inayomtafuna Rose juu ya kuwa teja. Madai yalikuwa ni kwamba Rose anatumia madawa ya kulevya ambayo yamemfanya kuwa mgonjwa, kukongoroka na kudhoofu mwili kiasi cha kutokuwa na tofauti na mateja wengine mitaani.
AANGUA KILIO
Kabla ya kujibu swali hilo, mara tu baada ya Wikienda kujitambulisha, Rose alianza kuangua kilio kwa uchungu na sauti ya juu akilalamika kuwa anaumwa sana na ameshahangaika na maisha haya bila msaada wowote na kwamba ameshatumika sana kutajirisha watu.
Ili mahojiano hayo yafanyike kwa utulivu, ilibidi kumtuliza kwanza Rose aliyeonesha kuwa na jazba mno.
Baada ya kutulia kidogo huku akiendelea kulia kwa kwikwi na kuombwa kunyamaza kila dakika, aliulizwa kinachomsibu ambapo alisema kuwa, anateswa na Ugonjwa wa Typhoid (Homa ya Matumbo) na mwili kuuma na kukosa nguvu hivyo kujiuguza mwenyewe nyumbani kwake, Ipagala, nje kidogo ya Mji wa Dodoma bila msaada.
ATISHIWA KUUAWA
Rose akasema muda mrefu sasa amekuwa akitishiwa kuuawa huku akipokea kichapo cha polisi ambacho humsababisha kuzimia, kwa kile alichodai kukataa kulala kwa maana ya kufanya ngono na mtu huyo.
Kwa mujibu wa Rose, amefikia hapo alipo kwa sababu alikataa kutekeleza jambo hilo kwa kuwa mhusika ni mume wa mtu na kwamba hata kama angekuwa si mume wa mtu, lakini huwa hana muda na mambo hayo.
Rose, bila kumtaja mhusika, anasema kuna mtu aliwahi kumsaidia kuingia studio kurekodi baadhi ya albamu zake, kwa sharti la kulala naye, lakini alipokataa ndipo manyanyaso na vitisho dhidi yake kutoka kwa mtu huyo vikaanza.
ANYANG’ANYWA MALI
Kwa mujibu wa Rose, mtu huyo aliwahi kudiriki kumnyang’anya mali zake, yakiwemo magari na vitu vingine vya thamani.
Rose alikaririwa: “Kwa kuwa anafahamiana na polisi, wakuu wa vituo vya polisi na viongozi wa dini, inakuwa rahisi kunisingizia mambo mengi machafu.
“Situmii madawa ya kulevya na sitatumia. Kama aliona ndiyo skendo itakayo-nimaliza, najua atashindwa, anayefanya hivyo ni mtu anayetaka kunimaliza, alitaka niwe mtu wake wa ngono na kumfanyia kazi, nikakataa.
“Sijawahi kujiingiza kwenya madawa ya kulevya na anavyozungumza, nasikitika kwa sababu anaiumiza familia yangu kisaikolojia.
“Mimi ni mama wa watoto watatu (Gift, Nicolas na Maximilian) na nina ndugu zangu, nasingiziwa mambo hayo kwa sababu sina mtetezi lakini ni vyema akajua mtetezi wangu ni Mungu.
“Lakini hii yote ni kwa kuwa nimekataa kulala naye. Napigwa hadi nazimia, wanaume walinizalisha na kunitelekeza, wameniumiza sana, afadhali ningefanyiwa mambo hayo na wanawake wenzangu, sasa natishiwa kifo, natamani hata kuhama nchi, hivi kweli akiona ninaishi nchini Kenya, ndiyo furaha yake?
“Lakini Mungu yupo na mbingu zitafunguka. Amekuwa akinizushia maneno makali, wakati mwingine nashinda porini, nikitetea maisha yangu.
“Kiukweli nimechoka jamani, acheni nipumzike, lakini namuachia Mungu, mbingu zitafunguka.”
MASWALI SAKATA LA ROSE
Baada ya hayo ndipo yakaibuka maswali juu ya sakata la Rose. Kama Ijumaa Wikienda tukawa tunajiuliza;
Je, ni nani huyo mwenye ubavu wa kutishia kutoa uhai wa binadamu mwenzake, achilia mbali Rose ambaye ni staa mkubwa kwenye jamii? Ni kosa gani alilolitenda Rose ambalo adhabu yake ni kifo?
Je, sababu ni hiyo pekee ya kumkataa kimapenzi au kuna sababu nyingine? Na je, mwanamke kumkataa mwanaume adhabu yake ni kifo? Nani kasema? Anamtishia kivipi? Kwa simu? Uso kwa uso? Wakiwa wapi?
Rose anasema amechoka kupelekwa kwenye vituo vya polisi ambako huko huwa anapigwa hadi anazimia, je, ni vituo gani vya polisi vilivyomfanyia hivyo ambavyo anaogopa kuvitaja kwa usalama wake?
Mara kadhaa Rose amekuwa akiripotiwa akidaiwa kutapeli watu kwa kuchukua fedha kisha kuingia mitini na kushindwa kufika kwenye matamasha. Kuhusu hilo Rose anahoji mbona hawajawahi kumfikisha mahakamani na aka-hukumiwa kama siyo kumchafua? Kama ni kweli huwa anatapeli, ina maana kesi zote wahusika humsamehe au hazifikishwi mahakamani?
HAPA KUNA TATIZO
Hapa kuna tatizo kubwa ambalo Rose anapaswa kuwa wazi ili kupata ufumbuzi na kumfanya aishi kama binadamu wengine na siyo kukimbilia porini ili kunusuru roho yake kama anavyosema. Ikumbukwe kuwa kila binadamu ana haki ya kuishi na siyo kuwindwa.
Nani Anataka Kumuua Rose Muhando?
Reviewed by Erasto Paul
on
May 15, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili