Hutoona tena sura ya Makonda kwenye TV na magazeti wala kusikia sauti yake redioni – Jukwaa la Wahariri

Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) limeamua kwa kauli moja kutokuandika au kutangaza habari zozote zinazomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Kuanza sasa, mikutano yake, shughuli zote anazozifanya Dar es Salaam hatutakwenda wala kuripoti chochote,” amesema Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kama kutakuwa na shughuli ambayo inahusisha kiongozi mwingine pamoja na Makonda, vyombo vya habari vitaripoti bila kumhusisha kwa vyovyote mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.
“Makonda tutampa total black out ni kazi rahisi tu,” amesema.

“Hatutarajii kuona sura yake kwenye televisheni, hatutarajii kuona sura yake kwenye gazeti wala kusikia sauti yake kwenye redio,” amesisitiza.

Kwenye taarifa yake, TEF imelaani vikali kitendo cha Makonda kuvamia kituo cha Utangazaji cha Clouds Media Group usiku wa Machi 17 akiwa na askari wenye silaha.

“Tunaalani vitendo vya Makonda na atakayekiuka na kufanya kazi na Makonda, kitakachomkuta hatutamsaidia. Waandishi,wahariri wote tunakubaliana, sote tunasema halikubaliki na tunalaani vikali vitendo vya Makonda, utekelezaji agizo la kutokufanya kazi na RC Dar unaanza mara moja kwa vyombo vyote vya habari nchini, uamuzi huu unaungwa mkono na UTPC.”

“Kwa mantiki hiyo, tunamtangaza Ndugu Paul Makonda kuwa ni adui wa Uhuru wa Habari, na yeyote yule atakayeshirikiana naye katika kukandamiza uhuru wa habari nchini,” imesema taarifa hiyo ya TEF iliyoandikwa na Mwenyekiti wake, Theophil Makunga.

Na Emmy Mwaipopo
Hutoona tena sura ya Makonda kwenye TV na magazeti wala kusikia sauti yake redioni – Jukwaa la Wahariri Hutoona tena sura ya Makonda kwenye TV na magazeti wala kusikia sauti yake redioni – Jukwaa la Wahariri Reviewed by Erasto Paul on March 22, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.