Upo ule usemi kwamba ukitaka kumficha jambo mtu mweusi basi weka ujumbe kwenye vitabu, hawezi kuuona na eti hilo ni jibu kwamba waafrika hatuna utaratibu wa kusoma vitabu. Hii ni tofauti kwa mwanasiasa maarufu na mbunge wa Kigoma Ujiji, Zitto Zubeir Kabwe ambaye mpaka kufikia sasa ameshasoma vitabu 53.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto amevitaja vitabu vyote na sababu za yeye kusoma vitabu hivyo pamoja na kile alichojifunza kwenye kila kitabu.
“Mwaka
2016 nimesoma vitabu 53. Nimeongeza vitabu nilivyosoma tofauti na mwaka
2015 lakini sikuweza kufikia idadi ya mwaka 2014 ambapo nilisoma vitabu
56. Hiyo ndio rekodi ya juu zaidi tangu nilipoanza kuorodhesha vitabu
nilivyosoma mnamo mwaka 2012. Mwaka 2013 niliorodhesha vitabu vichache
zaidi nilivyosoma.
Mafanikio
makubwa ya mwaka huu ni kuongeza vitabu vya Riwaya (fiction), ingawa
mtaona mwandishi mmoja, Jeffrey Archer amejitokeza sana kuliko wengine.
Hiyo ni kutokana na kusoma kazi yake moja nzuri na yenye mafunzo mengi
sana kwa wanasiasa iitwayo First Among Equals.
Kazi
hiyo ilinifungua macho na kuanza kusoma Clifton Chronicles (vitabu 7) na
kufuatia mapendekezo ya wanaonifuata kwenye mtandao wa kijamii wa
Instagram niliweza kupata vitabu vingine vya mwandishi huyu. Kwangu mimi
Bwana Jeffrey Archer ni Mwandishi wa Riwaya Bora wa Mwaka 2016.
Licha
kutaka kuanza na Gavana Ben Bernanke, nilijikuta naanza na vitabu kuhusu
Russia na Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin. Msukumo huo ulitokana na
namna nilivyomsoma Mtawala mpya wa Tanzania Rais John Magufuli
kulinganisha na Kiongozi wa zamani wa nchi yetu Rais Jakaya Kikwete.
Kitabu
nilichoanza nacho mwaka 2016 ni The Strongman: Vladimir Putin and the
Struggle for Russia kilichoandikwa na Angus Roxburgh. Baada ya kusoma
kitabu hiki nilijikuta ninanunua vitabu vingi kuhusu Urusi, Putin,
Udikteta, Demokrasia na Maendeleo ili kuweza kuelewa mwelekeo wa Siasa
za Tanzania za sasa.
Vitabu
hivyo vimenisaidia sana kujua namna ya kutafsiri watawala wapya kiasi
cha kuunda neno Dikteta Mamboleo (neo-dictatorship) na kuipa tafsiri
yake mnamo tarehe 29 Septemba 2016; kwamba Dikteta Mamboleo ni mtawala
ambaye ana uzalendo usio tiliwa shaka na anahangaika kuleta maendeleo ya
nchi yake lakini hataki kuhojiwa kwa namna yeyote ile.
Mwaka
2016 pia ulinifunua kuhusu uwezo mkubwa na umahiri wa wachapishaji wa
Vitabu wa ndani. Nilipata fursa adhimu ya kuzungumza na Mzee Walter
Bgoya wa Mkuki na Nyota Publishers. Vitabu kadhaa nilivyosoma katika
orodha ya mwaka huu vimechapishwa na Mkuki na Nyota. Nilijifunza mengi
mapya ya historia ya nchi yetu na Afrika nzima. Juzuu za masimulizi ya
Ukombozi wa Kusini mwa Afrika nilizipata kutoka Mkuki na Nyota na humo
nilipata mambo mapya mengi sana.
Kisa
kimoja kinachonichekesha kila nikumbukapo ni hadithi ya Rais Khama
(baba) wa Botswana alivyobeba machungwa kwenye ndege kumletea zawadi
Mwalimu Nyerere akimtania kuwa sera zake za Ujamaa zilileta njaa nchini.
Mwaka huu
ninawawekea mapema vitabu nilivyosoma tofauti na miaka iliyopita kwa
sababu kwa uwezo wake Manani sitaweza kusoma vitabu vingine baada ya leo
kwani nitakuwa na majukumu ya malezi. Karibu kwenye orodha ya vitabu
vyangu mwaka 2016″.
Orodha ya vitabu alivyosoma Zitto Kabwe mwaka 2016
Reviewed by Erasto Paul
on
December 20, 2016
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili