WATU
wawili wamekufa huku wengine wanne wakijeruhiwa baada ya majambazi
walio na silaha kuvamia mgodi wa dhahabu wa Nholi uliopo wilaya ya Bahi
mkoani Dodoma.
Majambazi hao wanadaiwa kupora dhahabu, fedha na mali nyingine na kuwavua watu nguo na kuondoka nazo.
Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Charles Kiologwe alikiri kupokelewa kwa
miili ya watu wawili hospitalini hapo na majeruhi wanne.
Alisema
mwili mmoja upo katika hali mbaya. Waliofariki dunia katika tukio hilo,
walitajwa kuwa ni Lukumale Membo na mwingine aliyefahamika kwa jina
moja la Hamisi.
Kwa
mujibu wa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,
Melisiana Danford, maiti hao na majeruhi walipokelewa hospitalini hapo
saa 6 usiku kuamkia jana mara tu baada ya kutokea kwa tukio hilo.
Majeruhi katika tukio hilo ni Sunday Undi (49), Lawrence Mhagama (35) ,
Maila Mchele (44) na Sophia Sayuni (37).
Wakizungumza
katika wodi namba moja ambako wamelazwa, majeruhi hao walisema
walivamiwa na majambazi, ambao baadaye waliwapiga risasi na kusababisha
vifo vya watu wawili na wengine kujeruhiwa.
Lawrence
Mhagama ambaye amepigwa risasi mguu wa kushoto, alisema amekuwa
akiendesha shughuli za uchimbaji mdogo kwenye mgodi huo. Alisema siku ya
tukio majira ya saa mbili usiku akiwa ndani, alisikia milio ya risasi
nje na alipojaribu kutoka, alipigwa risasi ambayo ilimjeruhi mguuni.
“Chanzo
cha tukio kwa kweli sikijui ila majambazi walituvamia , mimi ni mgeni
eneo hilo nilikwenda kwa ajili ya kazi ya mgodi, nimepigwa risasi mguuni
ambapo mpaka sasa bado ninayo mwilini, wanasema wataniruhusu nikipata
nafuu na baadaye wataangalia uwezekano wa kuitoa risasi hiyo,” alisema.
Alisema majambazi hao, walipora mali nyingi ambapo waliwavua watu nguo na kuondoka nazo huku wakiacha watu uchi.
Majeruhi
mwingine aliyelazwa wodi namba moja, Sunday Undi, alisema walivamiwa na
majambazi hao majira ya saa mbili kasorobo usiku wa kuamkia juzi,
wakiwa kwenye kioski cha Maila Mchele, wakipata vinywaji na kuendelea na
mazungumzo.
“Tulivamiwa
tukasikia tunaambiwa tuko chini ya ulinzi, kwa vile lilikuwa ni tukio
la kushtukiza tukawa tunashangaa, wakapiga risasi juu ikabidi tuingie
ndani ya kibanda kile baada ya muda tukajikuta watu saba tukiwa chini ya
kitanda,” alisema.
Alisema majambazi hao waliwaamrisha watoke na kuwaambia kila mtu atoe alichonacho na aliyekuwa akikataa, aliamriwa kuvua nguo.
“Walininyang’anya
fedha na simu, wakatuvua na suruali wakaondoka nazo, mimi binafsi
wamenipora Shilingi milioni mbili nilizokuwa nazo,” alisema.
Alisema
majambazi hao walikuwa zaidi ya wanne na walikuwa wamevalia kininja.
Alisema mtu aliyejaribu kuwatazama usoni, alikuwa akipigwa risasi.
Majeruhi mwingine katika tukio hilo, Maila Mchele ambaye amelazwa wodi
hiyo akiwa hajitambui, amejeruhiwa vibaya.
Inadaiwa
alipigwa risasi tumboni na kutokea upande wa pili. Majeruhi wa nne,
Sophia Sayuni (37) amelazwa wodi namba 10 hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alisema atalitolea ufafanuzi baadaye.
Majambazi Yavamia Mgodi na Kuua Watu Wawili
Reviewed by Erasto Paul
on
December 25, 2016
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili