Picha inamuonyesha Staa wa Bongo Fleva, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, akiandaa madawa kwa ajili ya kuvuta.
Akiwa katika chumba cha habari cha gazeti hili, mwezi mmoja uliopita, Chid Benz alisimama katikati na kusisitiza kuwa ameachana na utumiaji wa madawa ya kulevya na kwamba anajutia sana kitendo hicho ambacho kimeiacha familia yake ikimlilia. Kuthibitisha anachokisema, mkali huyo wa kibao cha Dar es Salaam Stand Up, alisema hakuna teja anayeweza kukaa chumba chenye kipoza hewa (AC) kwa muda aliokaa yeye (takriban saa nzima akiwa amesimama).
Lakini siku chache zilizopita, habari zilizagaa kwamba rapa huyo ambaye anapenda kujiita King Kong, amerejea katika matumizi ya mihadarati na tena kwa kasi kubwa.
Gazeti hili liliamua kuwasiliana na Kitengo Maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ili kiweze kuuthibitishia umma udanganyifu ambao msanii huyo aliwaambia mashabiki wake ambapo kilimsaka kwa siku mbili.
KINONDONI KWA MANYANYA
Taarifa za awali zilidai kwamba Chid, ambaye enzi zake alikuwa na mwili mkubwa, mkakamavu, akitajwa pia kuwa mkorofi na mwepesi kuwapiga wenzie, alikuwa akipatikana mitaa ya Kinondoni Manyanya, katika kituo cha mabasi ya daladala yaendayo Posta na makazi yake ni katika gheto moja lililopo umbali mchache kutoka hapo mtaa unaofahamika kama Brazil.
Watu kadhaa wanaofanya shughuli zao katika mitaa ya Manyanya, ambao waliulizwa kama Chid Benz anapatikana mitaa hiyo, walisema mwanamuziki huyo aliyepata kuwa kinara wa kushirikishwa kutokana na ubora wa sauti zake, ni kama mkazi wa maeneo hayo, kwani anapatikana mara kwa mara.
Baadhi ya vilevi pamoja na vifaa anavyotumika kwa ajili ya kuvutia madawa.
MSAKO MKALI WAMNASA MFADHILI WAKE GHETOBaada ya kuelezwa juu ya upatikanaji wake, OFM waliweka kambi katika eneo hilo ili liweze kumnasa, lakini kwa zaidi ya saa mbili halikuweza kumpata na lilipohoji mara ya mwisho kuonekana mitaa hiyo, likaambiwa ni siku mbili zilizopita. Kuona hivyo, wakaanza kutafuta gheto analodaiwa kuishi.
Baada ya mzunguko mrefu wa pandisha, shusha, kushoto kulia, hatimaye walifanikiwa kufika katika gheto analodaiwa kuishi na kufanikiwa kukutana na mtu anayedaiwa kumfadhili. Mtu huyo, ambaye jina na picha yake inahifadhiwa kwa sasa, alifanya mahojiano mafupi na OFM.
SWALI: Ni kweli Chid Benz anaishi hapa kwako?
JAMAA: Ni kweli Chid alikuwa anaishi hapa, mimi nilikuwa ninamhifadhi kama mshikaji wangu, maana tumewahi kuwa karibu kipindi cha nyuma. Lakini leo (Jumamosi) nimemwambia aondoke kutokana na kuonyesha kuwa msumbufu kwa wapangaji wangu hapa.
SWALI: Hebu funguka vizuri, usumbufu huo ni wa aina gani?
JAMAA: Si unajua tena yale mambo yake, akishapata au akiwa anapata anakuwa msumbufu sana, mara aanze kuimba kwa sauti ya juu, yaani ni kero tupu, kiukweli ndiyo maana mimi niliamua kumwambia atafute eneo lingine la kuishi.
SWALI: Mambo yake yapi, unamaanisha amerudia unga?
JAMAA: Aaah! Kwani hilo nalo siri, wewe zunguka Kinondoni nzima, kila mtu atakwambia Chid anatumia madawa, mimi siongei kwa ubaya lakini nahitaji asaidiwe maana anakoelekea si kuzuri. Kwa taarifa yenu tu, muda mwingine huwa anavuta na kuzima (kupoteza fahamu) hadi siku tatu.
SWALI: Upo karibu na Chid, unaweza kueleza pesa ya kuvuta unga anaipata wapi?
JAMAA: Kwa marafiki zake, unajua yule mtu wa watu na ni maarufu kwa hiyo hawezi kukosa pesa ya kununulia.
SWALI: Ni kama shilingi ngapi anatumia kwa siku katika kununulia unga?
JAMAA: Inaweza kufika laki mbili, maana ya shilingi elfu kumi yule hatosheki.
SWALI: Ni aina gani ya unga anaotumia?
JAMAA: Anatumia Pele na Msharifu.
SWALI: Dah, kwa hiyo kwa sasa anaweza kuwa yupo wapi?
JAMAA: Yaani ametoka hapa kama dakika tano tu, lakini yupo humuhumu Kinondoni, mkiamua kumsaka mtampata.
KIJIWE BAADA YA KIJIWE
OFM lilimuomba rafiki huyo wa Chid kumdokeza baadhi ya vijiwe ambavyo wanaweza kumpata, naye bila hiyana akawatajia na hivyo makamanda kuanza zoezi hilo. Wakiongozwa na mzoefu wa vijiwe hivyo, waliweza kupita kimoja baada ya kingine.
Katika sakasaka hiyo iliyochukua zaidi ya saa tano, OFM halikuweza kumpata msanii huyo ambaye pia aliwahi kuwa kiongozi wa kundi lake la La Familia na nusanusa, zikaonyesha kuwa alikuwa amepangiwa chumba katika hoteli moja maarufu mitaa ya Kinondoni Studio (jina linahifadhiwa). Waliompangia, wanadaiwa kuwa ni watu ambao walikuwa wanataka shoo wakati wa krisimasi katika eneo moja lililo nje ya jiji.
Baada ya kupata uhakika huo, mishale ya saa mbili usiku OFM ilipiga kambi kwa nje ya hoteli hiyo na saa nne usiku, rapa huyo mwenye sauti nzito, alionekana kwa mbali akiisogelea, akitembea kwa miguu.
Chid anasikitisha sana, akiwa na mavazi duni, suruali ya jeans na fulana, chini amevaa kandambili na katika mkono wake wa kulia akiwa amefungwa bandeji, kitu kinachoashiria kuwa alikuwa na jeraha, nyota huyo alisogea taratibu.
DAH, KUMBE CHID ANAUMWA HERNIA
Aliposogea, OFM lilimlaki kwa shangwe na kumchangamkia kiasi kilichomfanya atulie, akae chini na kuanza kupiga stori kwa zaidi ya saa moja, huku mara kwa mara akilalamika kuwa anaumwa sana ugonjwa wa Hernia na pia uvimbe chini ya kitovu ambao unamsababishia maumivu makali.
Chid alikuwa ameshika karatasi mkononi iliyoandikwa namba za simu za prodyuza Lamar ikadondoka chini, katika hali ya kushangaza alishindwa kuiokota maana kila alipoinama alihisi maumivu makali. OFM wakamsaidi a kuokota karatasi hiyo.
Chid: Washikaji msione nipo hivi lakini kiukweli ninaumwa sana, ninaweza kufa muda wowote, huu uvimbe chini ya kitovu unaniuma sana (akatoa wembe na kutaka kuuchana huo uvimbe, OFM mmoja alimdaka na kumsihi asifanye hivyo, akakubali baada ya kubembelezwa kwa muda).
OFM: Lakini kwa nini sasa unabwia unga na upo katika hali hii?
Chid Benz: Uvimbe huu ndio unasababisha, nisipobwia unaniuma mno, sasa huwa nautuliza kwa kuvuta.
NDANI YA CHUMBA CHAKE HOTELINI
Baada ya maongezi ya muda mrefu, Chid aliwaamini wageni wake kiasi cha kuwakaribisha chumbani kwake, kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo. Chumbani, OFM walishangaa kumuona Chid akitoa mfuko chini ya godoro, ambao ndani yake kulikuwa na sigara, wembe, kipande cha kigae, mirija na kopo la soda lenye maji nusu, likiwa limetobolewa na mrija kupitishwa.
Baada ya kutoa vifaa hivyo, Chid alikaa na kutoa kete za madawa ya kulevya na kuanza kuandaa kwa ajili ya kubwia. Huku akichukuliwa picha za video kwa uhodari wa hali ya juu bila kufahamu, mara mbili alishtukia kuwa anarekodiwa.
Lakini hata hivyo, kila aliposhtuka, alipoozwa kwa maneno matamu ya stori zikaendelea hadi saa tisa usiku.
OFM: Sasa Chid kwa nini hutaki kuachana na haya madawa wakati watu mbalimbali wanajaribu kukusaidia?
CHID: Aaah, nishawaambia ninaumwa, hata watu wanaonisaidia wamekwisha niambia niendelee tu kutumia taratibu lakini nijali uhai nisizidishe nisije kufa.
OFM: Kama watu wakitokea wanataka kukusaidia uache madawa utapenda wafanye nini?
CHID: Dah sijui hata wafanye nini, lakini labda wanisaidie nipate tiba ya haya magonjwa yanayonisumbua kidogo watakuwa wamenisaidia.
MASAI KLABU, SAA TISA USIKU
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, saa tisa usiku wote watatu walitoka chumbani hapo na akataka waelekee katika klabu ya usiku ya Masai.
BABU TALE ACHOMOA KUMZUNGUMZIA, KALAPINA AMLILIA
Watu wawili ambao awali walijitokeza kumsaidia kwa kumpeleka Sober House, Bagamoyo, Babu Tale na Kalapina walipotafutwa ili watoe maoni yao kutokana na kurudia kubwia unga, meneja wa kundi la Tip Top Connection, alikataa kumzungumzia.
Lakini Kalapina, ambaye pia ni msanii na mwanaharakati anayepinga matumizi ya madawa ya kulevya kwa wasanii, alionyesha masikitiko yake, akisema siku tatu zilizopita, alizungumza naye kwa simu, akimhakikishia kuwa ameacha kubwia.
“Alisema ameacha na kwamba kuna kamati maalum imeundwa kwa ajili ya kumsaidia, alinitajia majina yao Lamar na P Funk na wengine ambao siwafahamu. Nilimwambia achague vitu viwili, kutumia madawa au uhai wake, maana madawa yanaua.”
NINI KILIENDELEA?
OFM walienda na chid hadi klabu ya usiku ya Masai na huko akajichanganya na washkaji wengine. Katika gazeti la Risasi Jumamosi, tutakuletea simulizi ya mwisho ya mkasa huu wa kusikitisha wa nyota huyu mkali wa Bongo Fleva. Pia tembelea GLOBALTVTZ au kwenye mtandao kupitia www.globalpublishers.co.tz
KUTOKA KWA MHARIRI
Jamii haipaswi kukubali kushindwa na pengine imuelewe. Anasema ugonjwa wa Hernia anaoumwa, ndiyo unamfanya ale unga ili kupunguza maumivu makali anayopata. Ni vyema watu wake wa karibu wakamshauri na kumpeleka hospitalini ili atibiwe, kwa vile tunaamini baadhi ya madaktari wazuri ni mashabiki wa muziki wa Chid Benz.
Kwa muda ambao OFM walikaa na Chid Benz, alitumia unga wa karibu 60,000. Hii inaonyesha kuwa marafiki wanaompatia fedha, wanachangia kumfanya aendelee kutumia unga, ombi letu kwao ni kuwa, wajichangishe ili apatiwe matibabu ya magonjwa anayolalamikia.
Ikiwa Chid Benz yupo tayari kuondokana na hali hiyo Global Publishers ipo tayari kumsaidia na kushikamana naye mpaka arudi katika hali yake ya kawaida.
SOURCE; https://globalpublishers.co.tz/chid-benz/
Chid Benz Abambwa ‘live’ Akibwia Unga, Ndani ya Chumba cha Hoteli
Reviewed by Erasto Paul
on
December 28, 2016
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili