Wakati
majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold Corporation
kuhusu wizi unaodaiwa kufanywa kwenye uchimbaji na usafirishaji wa mchanga wa
madini (makinikia) yakiingia siku ya 64, Ikulu imesema majadiliano hayo
yanaendelea.
Majadiliano hayo yanafanyika kipindi ambacho Watanzania
wengi wana shauku ya kuona rasilimali za madini zinanufaisha Taifa.
Katika
majadiliano hayo yaliyoanza Julai 31, timu ya Tanzania inaongozwa na Waziri wa
Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Akizungumza
na Mwananchi leo Jumatatu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Gerson
Msigwa amesema majadiliano yanaendelea na wananchi wasubiri wataelezwa
kitakachojiri.
“Majadiliano
bado yanaendelea, wakiwa tayari watasema kwani hawawezi kuwa wanajadiliana mara
wanakwenda kusema katika media," amesema Msigwa.
Mazungumzo
hayo yalianza kufanyika kipindi ambacho Rais John Magufuli alikuwa
amekwishapiga marufuku ya kusafirisha nje makinikia hadi mgogoro wa kimaslahi
kati ya wawekezaji hao na Serikali utakapomalizika.
Miongoni
mwa kinachojadiliwa ni kodi ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeitaka
Kampuni ya Acacia kuilipa Serikali ya Tanzania Dola za Marekani Bilioni 190
ambazo ni zaidi ya Sh 434 trilioni zinazodaiwa kutokana na malimbikizo ya kodi
na adhabu.
Msingi
wa mazungumzo hayo ni baada ya Rais Magufuli kuunda tume mbili kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na
wawekezaji hao kwa zaidi ya miaka 19 iliyopita tangu walipoanza uzalishaji wa
dhahabu.
Majadiliano ya makinikia yanaendelea
Reviewed by Erasto Paul
on
October 02, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili