ANTONY Diallo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sahara Media Group (SMG), inayomiliki kituo cha televisheni Star TV, Redio Free Africa (RFA) na Kiss FM anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa kushindwa kulipa wafanyakazi mishahara.
Diallo atafikishwa katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kwa kushindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake 20 kiasi cha zaidi ya Sh. 100 milioni ikiwa ni malimbikizo ya kipindi cha miezi 16 sawa na mwaka mmoja na nusu.
Mahakama hiyo inatarajiwa kusikiliza mashauri 15 yote yakiwa ni ya kudai malimbikizo ya mishahara ambayo yatasikilizwa Julai 21 mwaka huu, ambayo tayari Tume ya Utumishi na Usuluhishi ulimuagiza Diallo kuwalipa lakini hakufanya hivyo.
Julai 13 mwaka huu, kampuni ya Diallo, ilifungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushindwa kulipa kodi ya Sh. 4.5 bilioni ambapo tayari wiki moja imekatika na taarifa zinadai hajalipa hata senti moja.
Katika hatua hiyo kampuni ilipewa siku 14 (wiki mbili) kuanzia Julai 13 mwaka huu, iwe imelipa kiasi hicho cha fedha na kama haitafanya hivyo majengo ya kampuni hiyo yanaweza kupigwa mnada ili kufidia deni hilo.
Diallo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, anadaiwa kiasi hicho cha fedha za malimbikizo ya kodi ya kipindi cha awali huku kipindi cha miaka miwili 2016/17.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo (jina linahifadhiwa) aliueleza Mtandao huu kuwa wamelazimika kumfikisha Mahakama Kuu baada ya kushindwa kutekeleza makubaliano yao, yaliotolewa na Tume ya Utumishi na Usuluhishi (CMA).
Mtoaji taarifa huyo ameeleza kwamba wanataka kuiomba mahakama kuagiza mara moja walipwe fedha zao mara moja na kwamba kama Diallo hana fedha pia Mahakama iangize wauze vitu vyake ili walipwe stahiki zao.
Amesema kuwa, kiongozi huyo ambaye alishawahi kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na baadae Waziri wa Maliasili na Utalii, amekuwa akiwatishia maisha kitendo kilichowalazimu wakaitafute haki yao mahakamani.
“Yeye amekuwa na dharau na kiburi kwa wafanyakazi wake na watu wengine, ndiyo maana hata kampuni yake ilifungiwa na TRA baada ya kupewa mwaka mmoja awe amelipa madeni yake lakini akafanya kiburi mpaka akafungiwa,” amesema mfanyakazi huyo.
Hata hivyo, alidai kwamba kitendo hicho cha kutolipwa mishahara kilisababisha baadhi ya wafanyakazi kupoteza maisha yao kwa msongo wa mawazo kutokana na kutengemewa na familia zao.
“Wanaolipwa pale mishahara ni wanawake tu, tena wale ambao hawana sifa lakini sisi wenye uwezo wa kufanya kazi hatulipwi mishahara yetu na tukihoji tunaonekana ni wachochezi, hali hii imetuchosha,” amesema.
Pia amedai kumekuwa na udanganyifu mkubwa unaofanywa na mwajiri kwa kutokupeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii PPF/NSSF na hata inayopelekwa imekuwa na taarifa za uongo ambayo michango inayowasilishwa hailingani na mishahara ya wafanyakazi.
Taarifa nyingine kutoka ndani ya kampuni hiyo zinaeleza kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imempunguzia masharti Diallo, badala ya kulipa deni la Sh. 4.5 bilioni, alipe Sh. Bilioni 2 ili wafunguwe kampuni hiyo lakini na yenyewe ameshindwa kulipa.
Kwa upande wake, Diallo, amekiri kuwepo na wafanyakazi wanaomdai lakini alidai hawazidi wawili huku akishindwa kuweka wazi kiasi wanachomdai.
Baada ya kufungiwa vituo vyake, Diallo aburuzwa mahakamani
Reviewed by Erasto Paul
on
July 19, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili