Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika
wa Mbinga, Leonard Kambo ambaye alidaiwa kuuawa na watu watano wa kanisa hilo
amekutwa akitoa ubatizo katika usharika wa KKKT Kitandilo, Makambako, Mkoani
Njombe.
Wakati Mchungaji huyo aliyedaiwa
kuuawa mwaka 2011 akionekana akitoa ubatizo kanisani, watu waliodaiwa kumuua
mchungaji huyo wamo mahabusu tangu mwaka huo 2011.
Ndugu wa watuhumiwa wa mauaji hayo
ndio waliohaha kusaka picha ya mchungaji huyo baada ya kupata taarifa kwamba
alihamishiwa eneo la Makambako baada ya kutokea tuhuma kwamba ameuawa.
Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya
ndugu kupata taarifa kwamba mchungaji huyo yupo hai, walitumia kila njia kupata
picha yake ili itumike kama ushahidi kwamba yupo hai na tuhuma dhidi ya wauaji
si za kweli.
Muumini mmoja wa kanisa hilo
alieleza kuwa ndugu wa watuhumiwa hao walihakikisha wanamnasa mchungaji huyo
kwa kamera popote alipo ili wasitishe kifungo cha ndugu zao na uongo dhidi yao.
Mmoja wa watuhumiwa wa kesi hiyo
ambaye alikamatwa kisha kuachiliwa huru, Leonard Myale alisema kuwa baada ya
kumuona na kupata picha ya mchungaji huyo akiwa hai, watathibitisha Polisi ili
akamatwe na watuhumiwa wengine waachiwe huru.
“Tumeteswa sana, tumedhalilishwa,
tumepuuzwa na kusemwa vibaya na Wakristo wenzetu, ndugu zetu na hata jamii
haikutuamini juu ya tuhuma hizi za uongo ambazo hata Polisi walitubambikiza
kesi bila kufanya utafiti wa kina. Tulikanusha kuhusika na mauaji hayo lakini
Polisi hawakutuamini. Sasa tunaamini tuko huru, wenye mamlaka watachukua hatua
za kutusaidia” alisema Elenia Mhoka mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo.
Aidha aliyewahi kuwa Mchungaji wa
KKKT Kitandililo, Geofrey Mtweve, alitafutwa ili kueleza kuhusiana na suala
hilo, lakini hakutaka kuzungumza chochote na kusema kuwa yeye siyo msemaji wa
kanisa hilo.
“Mimi si msemaji wa kanisa ila ni
kweli nilikuwa Kitandililo, uongozi umenihamisha kuja Ilembula, nimebadilishana
na Mchungaji Leonard Kambo, ambaye ndiye nimemkabidhi usharika, mengine
sifahamu lolote. Wasiliana na uongozi wa Jimbo,” alisema Mtweve.
Aidha mchungaji Kambo alipotafutwa
na kuulizwa kuhusiana na yeye kutuhumiwa kifo na kama ni kweli aeleze kuwa
alifufuka lini, lakini mawasiliano yakawa mabovu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
baada ya kuelezwa tukio hilo aliomba kupatiwa picha na namba ya RB na kuahidi
kuwa atalifanyia kazi suala hilo.
Mchungaji Aliyekufa 2011 Akutwa Akibatiza Kanisani Njombe;Washukiwa wa mauaji yake wapo Mahabusu.
Reviewed by Erasto Paul
on
May 04, 2017
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili