Wanaowamaliza Chid Benz, Nando Ni Hawa

 chidi-1-copy
Picha mbili juu zinamuonyesha Staa wa Bongo Fleva, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, akiandaa madawa kwa ajili ya kuvuta. 


 WIMBI la vijana kuzidi kutopea kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya ‘unga’ linazidi kuwa kubwa na safari hii, upepo mbaya umewakumba mastaa wa tasnia mbalimbali Bongo ambapo hali za kiafya za wasanii kama Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ na mwakilishi wa Tanzania kwenye Shindano la Big Brother, Ammy Nando zinasikitisha, chanzo kikiwa ni unga huo.
 
Picha zinazosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, zinawaonesha Chid Benz na Nando wakiwa taabani kiafya kiasi kwamba kama ulikuwa unawajua enzi za ‘uzima’ wao, leo unaweza kuwapita barabarani bila kuwatambua! Wamechoka, wanatia huruma.

MAGUFULI AOMBWA KUINGILIA KATI
Ni kutokana na hali za wakali hao ambao walikuwa wakifanya vyema hapo awali kabla ya kutumbukia kwenye safari ya mauti ya matumizi ya madawa ya kulevya, wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, wamepaza sauti kwa Prezidaa Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’  wakiuliza kwa nini yupo kimya wakati nguvukazi inateketea?

“Kwa kasi ya utendaji kazi wake, naamini Rais Magufuli hashindwi kufanya jambo kumaliza kabisa hili tatizo linalomaliza nguvu kazi ya taifa kila kukicha,” alisema msomaji mmoja wa Amani aliyejitambulisha kwa jina la Hamis Nandozi, mkazi wa Kimara Suka.
nando1
Mwakilishi wa Tanzania kwenye Shindano ya Big Brother Africa 2013, Nando. Muonekano wa sasa (kulia) na kushoto muonekano wake wa zamani.

WANAOWAMALIZA CHID BENZ, NANDO NI HAWA

Nandozi alisema kuwa, mbaya zaidi wanaomuuzia unga Chid Benz wanafahamika, waliomharibu  Nando wanafahamika na wanaowamaliza vijana mitaani pia wanafahamika. Why (kwa nini?) hawachukuliwi hatua? Tunamuomba Rais Magufuli aingilie kati sakata hili, anaweza kwa kuwa ndiyo mambo anayoyapatia sana ya kutatua kero za watu. Hii nayo ni kero.”

MAJINA YA WAUZA IKULU
Nandozi akaendelea: “Mimi nakumbuka niliwahi kumsikia rais aliyetangulia, Dk. Jakaya Kikwete ‘JK’ akisema kwamba wauza unga wote anawafahamu na tayari orodha ya majina yao ipo mikononi mwake. Mimi namuomba Rais Magufuli aipitie ile orodha kwa kuwa naamini JK hakuondoka nayo, awashughulikie wauza unga wote, wanaotuharibia vijana wetu.”

POLISI WABEBESHWA LAWAMA
Msomaji mwingine mkazi wa Shinyanga, Mathayo Kapalatu alisema kuwa, anawatupia lawama polisi kwa vile wao wana uwezo wa kuwasaka wauza unga na kuwatokomeza kwa kuwa mtandao wanaujua.

Alisema: “Polisi wanajua mpaka gari likiibwa, nani kaiba kwani wanajua wezi wa magari ya kifahari wako wapi, wezi wa magari makubwa wako wapi! Polisi wanajua wapi kunauzwa gongo, wapi kunauzwa unga, wapi kunauzwa bangi. Polisi wanajua hata kibaka akikata wavu wa dirisha, ule ukataji tu wanajua ni nani, sasa wanashindwaje jamani kuumaliza mtandao wa wauza unga?”

CHID BENZ
Ni mkali wa ngoma ya Dar es Salaam Stand Up, inadaiwa kwamba alianza kutumia madawa ya kulevya karibu miaka minne iliyopita lakini haikuwa rahisi kwa watu wa nje kumgundua, kwa sababu bado alikuwa anajimudu.

Hata hivyo, mambo yalianza kubumburuka Oktoba 24, 2014 alipokamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa safarini kuelekea Mbeya ambapo alikutwa na madawa ya kulevya aina ya heroin yenye thamani ya shilingi 38,638 na bangi ya shilingi 1,720.
chidi-3-copy
Baadhi ya vilevi pamoja na vifaa anavyotumika kwa ajili ya kuvutia madawa.

Aliburuzwa Mahakama ya Kisutu, Dar na kupigwa faini ya shilingi 900,000 na kuachiwa huru. Kuanzia hapo akawa hawezi kujificha tena, aliendelea kutumia unga ambao ulimfanya ‘akongoroke’ mwili, ule ubabe wake na mwili mkubwa aliokuwa nao, vyote vikayeyuka kama theluji iyeyukavyo juani.

Hali yake kwa sasa inasikitisha, anashinda mitaa ya Kinondoni, akiwa amepoteza kabisa unadhifu wake, kama unatembea na taswira ya yule Chid Benz wa kipindi kile, aliyekuwa anajiita King Kong, sasa amebadilika kabisa na kuwa mtu mwingine tofauti.

Juhudi zilizofanywa na Babu Tale na Kalapina na wengine, za kumpeleka sober house (nyumba ya kuwasaidia waathirika wa unga) zimegonga mwamba, ‘gari’ limewaka na hakuna wa kulizima mpaka Mheshimiwa Rais Magufuli atakapoamua kuingilia kati suala hilo.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alimtembelea mama yake Chiz Benz nyumbani kwake, Chanika wilayani Ilala, Dar kujaribu kuangalia namna ya kumsaidia kijana wake, lakini mpaka gazeti hili linaingia mitamboni, bado Chid Benz yupo mitaani akiendelea kujimaliza kwa kula ngada!


AMMY NANDO
Nando ni mwakilishi wa Tanzania kwenye Shindano ya Big Brother Africa 2013, ambaye alitolewa mjengoni baada ya kuhusika kwenye ugomvi mpaka kufikia hatua ya kumtishia mwenzake kisu, hali yake ni taabani kwa sasa! Huwezi kuamini kwamba ndiye yule ‘handsome boy’, aliyekuwa akipapatikiwa na wanawake.
nandoNando kabla ya kuathiriwa na madawa ya kulevya.

Nimewahi kufanya kazi kwa karibu na Nando, kipindi alichokuwa akifanya kazi ya uandishi wa habari mtandaoni. Nikiri kwamba ni miongoni mwa vijana wenye uelewa mkubwa mno! Anajua vitu vingi kuhusu teknolojia, historia, sanaa na mambo mbalimbali yanayoendelea duniani kote.

Makala zake alizokuwa akiandika ni ushahidi tosha wa  karama kubwa aliyojaliwa na Mungu. Hata hivyo, tangu awali alionesha kutokuwa sawa kwenye suala zima la matumizi ya vilevi.

 Alianza kama masihara, muda mwingi akipenda ‘kubugia’ pombe kali na kuvuta sigara, wakati mwingine hata wakati wa kazi.

Lakini kumbe ndiyo safari ilikuwa imeanza. Hakuishia hapo, akajiingiza kwenye mdomo wa mamba na kuanza ‘kula mambo’! Picha yake inayosambaa mtandaoni, imewashtua wengi, nikiwemo mimi. 

Ni vigumu kuamini kwamba ndiye yule Nando ninayemjua! Unga umemsambaratisha kabisa na kuua kipawa chake. 

Naamini Magufuli hawezi kukubali vijana ambao ni ‘taifa la leo’, wakiangamia hivi. Lazima atafanya kitu.

Hata hivyo, naamini Nando hajafikia hatua ya kuwa ‘chronic’ kihivyo, anaweza kusaidiwa na akarudi kwenye hali yake ya kawaida kwani hata watu wake wa karibu wanaeleza kwamba, akiwa hajapata mambo, anajitambua!

“Lakini kumsaidia yeye pekee haitoshi kwa sababu wapo vijana wengi nyuma yake, wanaopitia mapito kama yake! Dawa pekee ni kuwadhibiti wauza unga wanaowaharibu vijana hawa! Magufuli, where are you?” alisema msomaji mwingine, Salehe Njuguna, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam.

RAY C
Jitihada za rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete za kumsaidia Ray C ziligonga mwamba! Mwanadada huyu ambaye enzi zake alikuwa akisifika kwa jina la Kiuno Bila Mfupa kutokana na wimbo alioutunga kutamba enzi hizo, anaangamia. 

Licha ya mara kadhaa kujitokeza hadharani na kukiri kuacha kutumia madawa, kuna wakati aliendelea mpaka hivi karibuni ilipodaiwa ameacha na anajipanga kurudi kwenye gemu.

USHAURI KWA SERIKALI
“Mimi ushauri wangu, hawa wauzaji waundiwe sheria kali kama ilivyo nchi nyingine. Unajua China ukikamatwa na madawa ya kulevya, hakuna kumung’unya maneno ni kitanzi tu. 

Natamani hiyo sheria ije Bongo, vijana wetu wanaangamia wakati wauzaji wanabadilisha tu magari ya kifahari kila siku, leo Benz, kesho Vogue, keshokutwa BMW, lakini akina Chid wao tunawahesabia siku za kuishi, hapana! Inatosha sasa, Magufuli aingilie kati,” alisema mzee Juma Msongo, wa Temeke jijini hapa.

Akaendelea: “Hivi inashindikana nini polisi kuingia mtaani na kuwakamata akina Chid ili waende wakaonesha wanaponunulia madawa ambao nao wataonesha kwa mawakala wao wakubwa mpaka wa kwanza kabisa? Mbona rahisi tu.”
Wanaowamaliza Chid Benz, Nando Ni Hawa Wanaowamaliza Chid Benz, Nando Ni Hawa Reviewed by Erasto Paul on January 05, 2017 Rating: 5

No comments:

Thank you for commenting to Mwanauswahili

Powered by Blogger.