Mkazi
wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) afariki dunia
baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na
wananchi.
Komba
alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso)
ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo
nyoka wake huyo.
Mashuhuda
wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi
wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake
hilo halikusikilizwa.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki
ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za
usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia
tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani
barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu
kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na
kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule
alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na
kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka
ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza
kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana
waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la
kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige
kelele.
Alisema
kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana
hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake
kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na
maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa
kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema
wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo
naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu
mdomoni na puani.
Habari
zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili
ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa
hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote
na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya
rufaa Songea.
Alisema
nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na
uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio
hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda
Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea
vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Ruvuma.
Aidha
Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki
nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au
vifo.
Kijana afariki dunia baada ya Nyoka wake kupigwa hadi kufa
Reviewed by Erasto Paul
on
December 28, 2016
Rating:
No comments:
Thank you for commenting to Mwanauswahili